CHAMA cha Wajasiriamali wa Chuma Chakavu (WCC-Beach Kidimbwi), kilichokuwa ndani ya eneo la Kiwanda cha Nguo cha Urafiki (FTC), Ubungo, Dar es Salaam, kimelalamikia kitendo cha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuwataka walipe kodi ya ardhi katika eneo la biashara ambalo walijenga vibanda kwa makubaliano na kiwanda.
Aidha, kimelitaka shirika hilo kutambua uwekezaji walioufanya kwa kujenga fremu za biashara 12 zilizogharimu Sh. milioni 159 kwa makubaliano na uongozi wa FTC ili wanufaike na uwekezaji huo.
Mei 17, 2024 kupitia vyombo vya habari, NHC iliutaarifu umma kuwa imenunua eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya hekari 50, kwa mnada wa wazi wenye thamani ya Shilingi bilioni tatu, ikijumuisha nyumba, maghala, viwanja vya wazi, viwanda na mali nyingine.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa chama hicho, Salum Abdallah, alisema walianza kuuza vifaa vya vyuma chakavu katika eneo hilo mwaka 2004 na sehemu kubwa ilikuwa ni bwawa la maji, lakini kwa uhusiano mzuri waliokuwa nao na Kiwanda cha Urafiki walitumia gharama zao kuziba eneo hilo hadi likawa rafiki kwa biashara.
Alisema kwa kuwa wafanyabiashara walikuwa na nia ya kufanya uwekezaji kwenye eneo hilo ambalo hapo awali lilikuwa na vibanda vidogo vya wafanyabiashara wa vyuma chakavu, uongozi wa Urafiki uliwashauri kuunda chama ili kuendeleza eneo hilo badala ya kufanya mtu mmoja mmoja, ndipo walipounda WCC.
Aprili 24, 2022 WCC iliomba kibali cha kufanya maboresho katika eneo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 177.4 iliyoko kwenye kiwanja namba 28456 kwa lengo la kuliendeleza na Julai 14, 2022 uongozi wa FTC uliwajibu kwa barua kuwa wameridhia ombi hilo kwa masharti ya kuwasilisha mchoro halisi wa ujenzi kabla ya kuanza utekelezaji na walifanya hivyo.
Alisema pia walifuatilia kibali kutoka Manispaa ya Ubungo cha kujenga ofisi za muda katika eneo hilo kama walivyokubaliana na FTC na ombi hilo liliokubaliwa kwa barua maalum Mei, 27, 2022.
Baaada ya kutimiza masharti chama hicho kilitumia akiba iliyopo kwenye akaunti yake ya benki Sh. milioni 159 na kujenga fremu za biashara 12 na kumaliza ujenzi Novemba 2023 na kuvipangisha Desemba, 2023.
Wakati wanajiandaa kuwasilisha taarifa ya gharama walizotumia kujenga katika eneo hilo kwa uongozi wa FTC, ili waingie makubaliano ya uwekezaji huo utadumu kwa muda gani kwa, uongozi wa kiwanda kiwanja hicho uliwataarifu wasubiri kwa kuwa eneo la kiwanda kwa sasa kipo chini ya NHC.
Alisema walishangaa Aprili 30, mwaka huu, shirika hilo bila kuzungumza na uongozi wa WCC waliwapelekea barua wapangaji waliowapangisha kwenye fremu walizojenga wakiwataarifu kuwa eneo hilo ni mali yao hivyo kodi ziwe zinalipwa NHC moja kwa moja.
“Wale wapangaji walishangaa na wakawaambia kuwa wanatambua fremu hizo ni mali ya WCC kwa sasa na ndio walioingia nao mkataba, lakini NHC wakawajibu kuwa hawatambui umiliki wetu sisi katika fremu hizo na kuwasisitiza kodi zote zilipwe kwao, jambo ambalo si sawa kwa sababu sisi tumewekeza pesa zetu na tumepangisha kwa miezi mitano tu na wao wakaingilia kati,” alisema.
Waliandika barua makao makuu ya NHC kuwaomba watambue uwekezaji wao, wakati wakisubiri majibu mwezi Oktoba, NHC mkoa wa Ubungo uliwapelekea form za kusaini mkataba kati yao ambao ulikuwa na mabadiliko, ikiwamo kuwapandishia kodi ya ardhi kutoka Sh. 6000 kwa mita za mraba walizokuwa wanalipa hapo awali hadi Sh. 30,000.
Kwa mujibu wa Abdallah, walipokea fomu hiyo, lakini bado hawajatia saini na kuirudisha kwa sababu wanasubiri majibu ya madai yao waliyopeleka makao makuu.
Hata hivyo Novemba, mosi, mwaka huu NHC Ubungo iliwapelekea barua ya notisi ya siku 30 ikiwataka walipe deni la kodi ya ardhi ya Sh. milioni 14 .07 ikiwa ni sawa na Sh. milioni 1.698 kwa mwezi na ikiwa hawatekeleza agizo hilo mpaka Novemba 30, mwaka huu NHC itawavunjia mkataba.
“Tuliamua kulipa sehemu ya kodi hiyo kama Shilingi milioni tatu hivi, ili kushikilia wasivunje mkataba wakati tunasubiri majibu kutoka makao makuu juu ya uwekezaji tuliofanya katika eneo hili,” alisema.
Katibu wa WCC, Festo Gabriel, alisema kuwa chama hicho hakina tatizo na kulipa kodi ya ardhi kwa kuwa ndicho walichokuwa wakifanya miaka yote wakati wapo chini ya FTC, wanachotaka wao ni uongozi wa NHC utambue uwekezaji walioufanya wa kujenga fremu 12 na wawaachie wanufaike.
UONGOZI URAFIKI
Meneja wa Kiwanda cha Urafiki, Thomas Mushi, amekiri kuwaruhusu WCC pamoja na wapangaji wengine kujenga fremu katika eneo hilo kwa makataba, lakini eneo hilo lilinunuliwa na NHC kwa mnada wa wazi na hafahamu sababu za shirika hilo kutotambua uwekezaji watu hao.
NHC YAJIBU
Meneja Habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya, alisema baada ya kulichukua eneo hilo walilifanyia tathmini na kuwahakiki wapangaji wote waliokuwa chini ya Urafiki na kuwaweka chini yao ili wakubaliane na taratibu za upangaji wa shirika hilo.
Alisema wakati wanafanya tathmini waligundua kuwa eneo hilo lina thamani kubwa kinachohitajika kufanyika ni maboresho, ikiwamo kuondoa vibanda katika baadhi ya maeneo na kujenga nyumba za kisasa ili liendane na thamani.
Alisema pia waligundua kuna vitu vingi vinaendelea ikiwamo watu kupangisha fremu kwa watu wengine na kupata faida zaidi jambo ambalo ni kinyume na taratibu za shirika hilo.
Alisema kwa upande wa WCC, shirika linatambua uwekezaji wao na limewapa eneo kubwa ambalo linatosha kufanyia shughuli zao na wanawatambua kuwa ni wapangaji wao, kama hawajaridhika na walichopewa wapeleke malalamiko yao kwenye shirika.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED