Dhuluma za mirathi zamshangaza waziri, waliolizwa wamjibu kwa ushuhuda mzito

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 07:16 PM Nov 26 2024
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima
Picha: Mtandao
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima

UJUMBE wa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, kuhusu kuandika wosia wa urithi wa mali, umezua gumzo mitandaoni huku wengine wakishuhudia namna walivyokutwa na madhila kwa kukosekana wosia.

“Ndugu zangu, kwa dhati ya moyo wangu mkiwa wanandoa, kubalianeni muweke mambo yenu ya mirathi vizuri, siku moja mmoja kati yenu akitangulia mbele za haki, kusiwe na heka heka ya migogoro ya kesi na kuathiri watoto.

Na pia kwa upande wenu wanaume, nyie ndio viongozi wa familia na hususani pale penye ndoa, uelewa wenu na sauti yenu ni muhimu sana kwenye uongozi na maamuzi haya, tafadhali, toeni uongozi mapema kwenye ajenda hi muhimu,” ulisomeka ujumbe wa Dk. Gwajima.

Alisisitiza mirathi hiyo inapaswa kuandikwa kwa waliooana au wasiooana isipokuwa kama wana watoto.

“Kama mmeoana na kuna watoto au hata bila watoto au hata kama hujaoa au kuolewa ila unao watoto, naomba andikeni mirathi yenu mapema kabisa ili mkitangulia au akitangulia mbele ya haki mmoja wenu wanandoa, msiache migogoro na kuacha watoto wenu kwenye mitihani. Tunapata changamoto sana kuhusu hizi kesi, mtakuja kukumbuka huu wosia.

“Kwa niliyoyasikia na kushuhudia katika kuhudumu kwenye hii Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kuna kesi nyingi mno za migogoro isiyo ya lazima kuhusu mirathi, watoto wanahangaika wakati mwingine bila sababu.

“Ndugu zangu, dunia imeshajaa hila na husda na fitina na tamaa za mali, ambazo mtu hazimhusu na umdhaniaye siye, anakuja kuwa yeye kabisa. Watoto wanaumia, mzazi aliyebaki na watoto anaumia, ni vilio, na mara nyingi ni wanawake na watoto ndio wanaumia hapa. Uzuri kuna programu nyingi za msaada wa kisheria kuhusu hizi huduma, tutumie fursa hizi,” aliandika Dk. Gwajima.

Baadhi ya watu walitoa maoni yao kwenye akaunti ya Dk. Gwajima akiwamo Mayenda Shabani, aliandika urithi utawafanya baadhi ya wanawake waanze kuua waume zao.

Rammy alisema: “Mama mbona kauli yako inalenga kwamba wanaume ndio tunatangulia kufa?”

Wakati Micho alisema mambo ya urithi yanachelewesha watu na kutaka kila mtu apambane mwenyewe.

Benny, alisema mali zake ataachia kanisa anakosali na kwamba mambo ya kurithisha mtu hapana.

Unique, alisema hasa wanaume ndio mali zao zote huandika majina ya mama zao.

Mrs Kayege alisema: “Mama umeniliza mimi, huu ujumbe umenigusa, yametukuta sisi kudhulumiwa haki zetu na baba mdogo kwa mambo kama haya hakika ushauri mzuri, asante mama.”

Kiyenze alisema: “Sana mama yangu, ila huwa hawaelewi kabisa. Mimi najionea sasa, baada ya kifo cha marehemu mume wangu, napitia mengi, sasa familia imeshavurugika kabisa yaani inafikia hatua mke wa ndoa wanakukataa, cha kushukuru Mungu ni kwa kuwa kuna ndoa halali inasaidia, sasa ambao hawana ndoa sijui inakuaje...tujitahidi kuandika wosia ili kuepuka migogoro.”

Vituko kitaani “Maandishi ya kisheria huwa yanadumu sana, maoni yangu urithi uandikwe maana ndio unabainisha kila kitu wazi.”

Advocate Lorrayne aliandika: “Umetoa ushaui mzuri sana waziri, kuandika wosia sio uchuro bali ni kupanga mali zako zitumikaje, unapokuwa haupo tena duniani, sote ni wapitaji, lolote linaweza kutokea na  popote ulipo na muda wowote na hasa familia zetu za kiafrika baadhi ya mila za desturi na dini.

“Tuna watoto kutoka kwenye mke zaidi ya mmoja ingawa hata wa mama mmoja nao pia wakati mwingine wanagombana. Lakini sasa sheria nazo kupitia maamuzi mbalimbali ya mahakama inaruhusu mtoto yeyote ili mradi upo ushahidi kuwa amezaliwa na baba wa mji basi naye ana haki, hilo nalo ni changamoto.

“Kwa kuwa wapo kinamama ambao wamechuma katika ndoa pamoja na inapotokea watoto ambao hawakutambulishwa kabla ya kifo cha mzee wa mji inakua changamoto, so na support kuwa tuseme na tuandike tu maelekezo yetu tukiwa hai.”

Endendekisye aliandika: “Lakini mama haya masuala yanahitaji sana mwongozo wa wanasheria, asilimia 90 ya Watanzania elimu ya sheria imetupita kushoto, ombi langu kwako mama kabla ya hatujafikia uamuzi tunaomba sana elimu itolewe juu ya issue nzima ya mirathi.”

Upendo Pallangyo alisema: “Mama umesema kweli tupu...Mume wangu alifariki 2021, tunasumbuana na ndugu zake vibaya mno, kesi ipo mahakamani... hili ni janga sana, nadhani ufanyike utaratibu iwe ni kama lazima kila familia ya mke na mume kwa ngazi ya familia na ukoo waambiane.