SERIKALI imeipatia Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Sh. bilioni 13.5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya taaluma ili kukabiliana na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na taasisi hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Pallangyo, alibainisha hayo juzi wakati wa mahafali ya 22 yaliyowahusisha wahitimu 1,477 wa kampasi hiyo.
Alisema kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga katika taasisi hiyo ambapo katika mwaka wa masomo 2024/25 wamelenga kudahili wanafunzi 1,600 na hadi sasa wameshadahiliwa 1,276.
Prof. Pallangyo alisema kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi kumetokana na utaratibu wa serikali kupitia TAMISEMI kuwapangia vyuo wahitimu wa kidato cha nne, ongezeko la wanufaika wa mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), kuanzishwa kwa shahada ya uzamili na ubora wa elimu unaozingatia umahiri wa mafunzo kwa vitendo.
Aidha, alisema taasisi hiyo imeandaa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi 52 kuhusu usimamizi wa fedha za umma, utawala bora na uongozi ambapo kampasi ya Singida imeendesha madarasa ya maandalizi ya mitihani ya Bodi ya Uhasibu (CPA) na Bodi ya Ununuzi na Ugavi (CSP).
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, aliwataka wahitimu kupenda kujiajiri hasa katika kipindi hiki ambacho taifa limeweka mazingira mazuri ya vijana kupata mitaji bila riba yoyote.
Dendego aliwasihi wahitimu kutumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kutangaza bunifu zao kwa kukutana na wateja na kueneza mawazo mapya ya kuliendeleza Taifa badala ya kupoteza muda mwingi kwenye mitandao kwa kujadili mambo yasiyo na manufaa.
Mjumbe wa Bodi ya Kiushauri Wizara ya Fedha, Renatus Msangira, alisema TIA kampasi ya Singida inatoa mafunzo kwa ufanisi na ushindani na kufanya tafiti zenye manufaa kwa jamii na nchi na kutoa ushauri wa kitaalamu katika fani za uhasibu, ugavi na nyingine.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED