MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), imewataka Watanzania kuendelea kuzingatia matumizi sahihi ya dawa na kuacha kutumia kiholela bila kufuata maelekezo na ushauri wa wataalamu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Fimbo amesema kuwa mamlaka hiyo inaendelea kupambana na usugu wa vimelea vya dawa na kuelimisha jamii katika kuhakikisha dawa zinatumika kwa ufasaha na usahihi kwakufuata maelekezo sahihi ya kitaalam.
“Usugu wa Dawa umekuwa ukiongezeka siku hadi siku kutokana na matumizi ambayo sio sahihi, nakupelekea wananchi wengi kupata madhara,” amesema.
Fimbo amesema TMDA imeshiriki maonesho ya Sabasaba mwaka huu ili kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya dawa na kufahamu majukumu ya taasisi hiyo.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutembelea kwenye banda lao kupata elimu ya udhibiti na matumizi sahihi ya dawa awa na vitenganishi.
“Tunawakaribisha wananchi wote wanaotembelea Sabasaba wapite banda la TMDA ili wajionee shughuli tunazofanya lakini pia tuwape ushauri kuhusu matumizi sahihi ya dawa ili kuepuka madhara,” amesema Fimbo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED