THRDC yaomba Sheria za Haki Jinai ziboreshwe kwa ustawi wa wafungwa na mahabusu

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 06:10 PM Nov 08 2024
Gereza la Loliondo mkoani Arusha.
Picha:Mpigapicha Wetu
Gereza la Loliondo mkoani Arusha.

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) yaomba kuimarishwa kwa Sheria za Haki Jinai kwa utoaji huduma kwa wafungwa na mahabusu nchini ili kuboresha haki za binadamu kwa makundi yote.

Hayo yalisemwa na Mratibu Kitaifa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa alipotembelea katika Gereza la Loliondo mkoani Arusha.

Olengurumwa ameiomba Serikali kuboresha zaidi mazingira katika magereza ikiwemo na mienendo ya sheria kwa wafungwa na mahabusu wawapo magerezani.

Akiwa katika gereza hilo THRDC kwa kushirikiana na Kituo cha Msaada wa Kisheria Ngorongoro (NGOLAC) waliweza kukabidhi magodoro na vifaa mbalimbali katika gereza hilo.

Mkuu wa gereza hilo, SP George Osindi, amesema kwa sasa gereza hilo lina jumla ya wafungwa 80 na mahabusu 21 na kubainisha kuwa Gereza hilo limejitosheza kwa asilimia 90 kwa upande wa maeneo ya kuhifadhi wafungwa.

Amesema Gereza la Loliondo ni moja ya magereza kongwe na lenye historia kubwa sana lilijengwa na kuanzishwa mwaka 1922, ikiwa ni gereza la tatu nchini Tanzania lililojengwa kabla ya Uhuru.

1

“Tunawashukuru sana THRDC na NGOLAC kwa msaada huu waliotuletea hapa kwani baadhi ya tulivyoletewa tulikuwa na uhitaji navyo, atunamba mashirika mengine wajitoe kama walivyojitoa hawa” amesema

Aidha Mratibu Olengurumwa yuko katika ziara ya kutembelea wanachama wa THRDC kwa Kanda ya Kaskazini (Manyara, Arusha na Kilimanjaro).

Ziara hiyo ina malengo mbalimbali, ikiwemo kutambua Sekretariet ya Mtandao kuona Ofisi za wanachama wake, kushuhudia kazi wanazozifanya mikoani na wilayani, kufahamu changamoto zinazowakabili na kuzijadili, na kukumbusha majukumu yao kama wanachama.

Vilevile alipata wasaa wa kutembelea Tarafa ya Ngorongoro kuona utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kurudisha huduma kwa jamii pamoja na vijiji vilivyofutiwa shughuli za uchaguzi.
2