TET, Soma Kwanza kuanza mradi wa "Elimu Kiganjani"

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 01:34 PM Nov 07 2024
TET, Soma Kwanza kuanza mradi wa "Elimu Kiganjani".
Picha: Mpigapicha Wetu
TET, Soma Kwanza kuanza mradi wa "Elimu Kiganjani".

TAASISI ya Elimu Tanzania (TET), kwa kushirikiana na Taasisi ya Soma Kwanza Initiative, wanatarajia kuanza kutekeleza mradi wa elimu kiganjani kwa kuanzisha redio, televisheni na mitandao ya kijamii, mahsusi kwa kusambaza maudhui ya elimu yaliyoandaliwa kitaalamu.

Mkurugenzi TET, Dk.Aneth Komba, amesema uandaaji wa maudhui ya vipindi hivyo  ambavyo vitakuwa vinarushwa kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(Tehama), vitazingatia mitaala ya elimu ya Tanzania. 

“Katika mitaala iliyoboreshwa, serikali imeimarisha matumizi ya Tehama na teknolojia nyingine katika ufundishaji na ujifunzaji, ujuzi wa kidijitali ambayo ni mojawapo ya stadi muhimu za karne ya 21, zimebainishwa bayana katika malengo makuu ya elimu nchini, hivyo programu hizo zitawekwa katika vitendo vya ufundishaji na ujifunzaji kwa masomo yote kuanzia ngazi ya elimu ya awali. 

“Makubaliano ambayo tumeyasaini leo, yamekuja wakati mwafaka wakati serikali inaendela kuimarisha matumizi ya Tehama katika ufundishajia na ujifunzaji,”amesema Dk.Aneth.

Amesema katika makubaliano yao baadhi ya majukumu ya TET yatakuwa kuratibu utekelezaji wa mradi kuhakikisha unafanyika kwa mujibu wa sera ya elimu ya nchi, kutoa nyaraka za mitaala na muhtasari, kushiriki katika uaandaaji wa maudhui ya kidigitali na kuidhinisha maudhui ya kidigitali yatakayoandaliwa. 

“Tutakuwa tunaongoza na kufanya ufuatiliaji na tathmini kwa kushirikiana na wadau wengine wanaohusika, kuandaa TET Soma Kwanza TV, Soma Kwanza Radio, na Soma Kwanza App na kutumia vyombo hivyo kwa ajili ya kusambaza taarifa za elimu,”amesema Dk.Aneth. 

“Baadhi ya majukumu ya Soma Kwanza initiative ni kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji mradi huu, kuwezesha ufuatiliaji na tathmini, kushirikiana na TET kuandaa maudhui ya elimu ya kidijitali na kusimamia utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya miradi.”

“Lengo na fahari yetu sote ni kuona mradi huu unafikia mafanikio yanayotarajiwa na kuchangia katika utekelezaji wa mitaala iliyoboreshwa.”

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Soma Kwanza, Peter Kangere, alisema wamefikia makubaliano hayo ya kuanzisha televisheni, radio pamoja na kusambaza maudhui mitandaoni mahsusi ya kutoka elimu kiteknolojia, baada ya kufanya utafiti kwa miaka minnne.

“Lengo kubwa ni kuwawezesha watoto kutoka katika familia zote bila kujali hali zao za kijamii na kiuchumi, kupata maudhui bora ya kielimu ya kusaidia kufikia hatma ya maisha.Dunia inazidi kuwa ya kidijitali kwa kutumia Tehama, tunataka kuhakikisha hawabaki nyuma katika mabadiliko haya,”amesema Kangere.

“Kama ilivyo dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutoa elimu bora na iliyo sawa kwa watoto wetu, hatua hii inalenga kuendeleza juhudi hizo za serikali kwa kutumia teknolojia na tunataka maudhui ya elimu yatakayosambazwa yawiane na  mitaala ya Tanzania  ili wanafunzi wa mijini na vijijini wapate elimu bora na kwa njia rahisi.”