TAZAMA yatoa gawio bil. 4.3/- kwa serikali

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:45 AM Aug 27 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko.
Picha:Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko.

SERIKALI imepokea gawio la Sh. bilioni 4.35 kutoka Shirika linalosimamia bomba la mafuta kutoka Tanzania kwenda Zambia (TAZAMA).

Akizungumza wakati wa kupokea hundi ya gawio hilo jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, alisifu hatua hiyo kuwa ni muhimu kwa Tanzania kwa kuwa mradi wa bomba hilo una miaka mingi na sasa matunda yanaonekana.

“Mara ya mwisho kutoa gawio kwa serikali ilikuwa miaka mitano iliyopita na sasa tumepokea fedha hizi, tunajivunia maana badala ya kuja na sababu na visingizio kadha wa kadha, lakini mmekuja na fedha, kuna baadhi ya taasisi wanakuja na maneno mengi ya kijanja…unajua kulikuwa na Covid, tatizo la dola, lakini nyie hamkuwa hivyo, tunatarajia wakati mwingine kutakuwa na habari njema zaidi,” alisema.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan alipotembelea Zambia, moja ya maelekezo yake ilikuwa ni miradi inayounganisha nchi hiyo na Tanzania isimamiwe vizuri ili ilete manufaa kwa nchi zote.

Alisema Samia alielekeza kwamba angefurahi kuona miradi kama TAZAMA inaleta siyo tu manufaa ya kikodi kwa nchi bali ichangie kunufaisha maisha ya watu.

Aliipongeza bodi na uongozi wa TAZAMA kwanza kwa kufanya jambo hilo liwezekane.

Aidha, Wizara ya Nishati iko kwenye mazungumzo ili kuongeza uwekezaji kwenye bomba la TAZAMA.

“Kama mnavyofahamu tunataka kupanua bomba lililopo kutoka nchi nane hadi 12 na litaanza muda si mrefu ili tusafirishe mafuta mengi kwenda Zambia na baadaye kutoka Zambia kwenda nchi za Kongo (DRC) na majirani zetu,” alisema.

Alisema wanakusudia kuanza ujenzi wa bomba jipya la inchi 24 na kwa sasa wapo kwenye hatua mbalimbali za ununuzi ili mafuta mengi zaidi yasafirishwe kwa bomba badala ya malori.

“Tunataka tuwe na vituo njiani kutokea hapa kwetu katikati kuwe na vituo vingi vya kutoa hayo mafuta mbadala yanayokwenda Kusini yapelekwe na lori sasa litumike bomba lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata mafuta bei nafuu sababu sehemu ya gharama kubwa inayosababisha bei kuongezeka pamoja na nyingine, lakini gharama za usafirishaji zinavyoendelea kuwa kubwa na kufanya mafuta yaendelee kuwa na bei kubwa,” alisema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema kuwa gawio hilo linadhihirisha namna ushirikiano wa Tanzania na Zambia ulivyo imara.

Awali, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu aliisifu TAZAMA na kusema sasa imeamka ikiwa na miaka takriban 58 tangu kuanzishwa.

Mchechu, alisema umri huo kama ni mtumishi wa umma amebakiza miaka miwili kustaafu na kwamba anakuwa kidogo mnyonge mnyonge.

“Lakini kwa TAZAMA badala ya kuwa mnyonge ndio imekuja juu, imekuwa tofauti kidogo,” alisisitiza.

Alisema mafanikio hayo ya TAZAMA ni moja ya faida za falsafa ya 4R za Rais Samia akimaanisha maridhiano, ustahamilivu, mageuzi na ujenzi mpya.

Mchechu, alisema mabadiliko ni makubwa kwa sababu yamekuwa kwa mpigo. “Kama mnavyoona na sisi tunatumia mageuzi na ujenzi mpya hapa napenda tumpongeze Rais Samia,” alisema Mchechu.

TAZAMA ilitoa gawio hilo kwa serikali jana baada ya kupita miaka mitano. Kwa mara ya mwisho ilitoa Sh. milioni 681.8 mwaka 2019.