Tanzania yawakuna vigogo WB, AfDB

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 08:01 AM Jan 28 2025
Rais wa Benki ya Dunia (WB), Ajay Banga
Picha: Mtandao
Rais wa Benki ya Dunia (WB), Ajay Banga

WAKUU wa taasisi za fedha ulimwenguni na Afrika wamesema upo uwezekano wa Bara la Afrika kubadilisha sura ya ukanda huo kupitia sekta ya nishati kwa kuweka nguvu ya pamoja kuunganisha rasilimali zilizopo kuhakikisha zinawafikia wananchi wengi ifikapo mwaka 2030.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Mkutano wa Nishati wa ‘Mission 300’ uliowaleta pamoja wakuu wa nchi 24, mawaziri na washiriki wengine zaidi ya 2,600 jijini Dar es Salaam jana, wakuu hao walisema ushirikiano baina ya nchi za Afrika utawezesha ajenda hiyo kufanikiwa.

Rais wa Benki ya Dunia (WB), Ajay Banga alisema lengo hilo ni gumu kulifikia lakini linatekelezeka kwa juhudi za pamoja.

"Idadi ya nchi zilizopo hapa si ndogo, kwa umoja wetu tukiweka nguvu za pamoja linatekelezeka," alisema Banga.

Rais wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), Dk. Akinumwi Adesina, alipongeza Tanzania kwa kufikisha nishati ya umeme hadi ngazi ya vijiji vipatavyo 12,318, akisema ni mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine.

Alisema hatua hiyo ambayo Tanzania imefikia inachangia kuchochea maendeleo na ustawi kwa wananchi vijijini.

"Nitumie fursa hii kumpongeza Rais wa Tanzania,Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha wananchi wa Tanzania kufikiwa na nishati ya umeme katika vijiji vyote, jambo hili linastahili kupongezwa kutokana na umuhimu wa nishati hii katika maendeleo," alisema Dk. Adesina.

Alisema lengo la mkutano huo ni kuhakikisha nishati hiyo inawafikia waafrika milioni 300 wanaoishi chini ya ukanda wa Jangwa la Sahara na kwamba lengo hilo linakwenda kufanikiwa ili kuifungua Afrika kupitia eneo hilo muhimu.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bo Li alisema shirika hilo liko tayari kufanya kazi na nchi za Afrika ili kusaidia Mission 300 kukamilika huku akiwataka wabia wengine kuunga mkono ajenda hiyo kuhakikisha inafanikiwa.

Mkutano wa Nishati Afrika unafanyika kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam, Tanzania ukiwakutanisha wakuu wa nchi za Afrika kwa  lengo la kuwafikishia nishati ya umeme waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.

Majadiliano ya jana yalihusisha mawaziri na wadau wa masuala ya nishati na fedha na leo yatahusisha ngazi ya viongozi wakuu wa nchi za Afrika.

Rais wa Benki ya Asia (AIIB), Jin Liqun aliahidi kuchangia Dola za Marekani bilioni 1.5 kwa ajili kuunga mkono jitihada za upatikanaji umeme kwa watu milioni 300 barani Afrika ifikapo mwaka 2030.

Mkutano huo wa wakuu wa nchi wa Afrika ulianza jana na unatarajiwa kufikia tamati leo.

Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko alisema Tanzania inauchukulia kama kichocheo cha utekelezaji Sera yake ya Taifa ya Nishati inayolenga kuendeleza nishati endelevu, uhifadhi na ufanisi.

Dk. Biteko alisema Tanzania inahitaji uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati kwa kuwa matarajio yake ni kukuza shughuli za kiuchumi hususan katika sekta za viwanda na madini.

Alisema Rais Samia amekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhisho la nishati safi ya kupikia barani Afrika, jitihada ambazo zimeungwa mkono na mkakati wa kitaifa na kujumuishwa katika azimio litakalotiwa saini katika mkutano huo leo.

Alisema ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025, uzalishaji umeme Tanzania utaongezeka hadi megawati 4,000, kutoka kwenye vyanzo safi.

Alitaja mambo yatakayofanyika katika mkutano huo kuwa ni pamoja na kufungua uwekezaji wa sekta binafsi, kuanzisha ushirikiano wa kufadhili miundombinu ya nishati na kukubaliana mfumo wa ufuatiliaji ikiwa ni pamoja na kuanzisha mpango wa kufuatilia maazimio ili kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye mkutano huo. 

"Ni matarajio yangu kwamba mamlaka zinazohusika za nishati katika kila nchi ya majaribio zitajitahidi kuhakikisha maazimio ya nishati yanafanikishwa kupitia malengo na mipango ya hatua zinazolenga kuongeza kiwango cha upatikanaji umeme, matumizi ya nishati safi ya kupikia, nishati mbadala na mchango wa sekta binafsi katika kufanikisha upatikanaji nishati hiyo," Dk. Biteko alihitimisha.