Watuhumiwa wa ubakaji, ulawiti wafungwa maisha jela

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:00 PM Feb 17 2025
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo
Picha:Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanikiwa katika operesheni maalum dhidi ya uhalifu na wahalifu, iliyofanyika kuanzia Januari hadi Februari 2025, ambapo watuhumiwa mbalimbali walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo, amesema kuwa katika operesheni hiyo, walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 15 wa makosa ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, kati yao 10 wakihusishwa na tuhuma za ubakaji na wengine watato (5) kwa ulawiti.

Kwa mujibu wa Kamanda Masejo, baada ya kufikishwa mahakamani, watuhumiwa watatu wa ubakaji wamehukumiwa kifungo cha maisha jela, mmoja kifungo cha miaka 30. Aidha, kwa makosa ya ulawiti, mtuhumiwa mmoja amepewa kifungo cha maisha, huku mwingine akihukumiwa kifungo cha miaka 30. Kesi za watuhumiwa wengine bado zipo katika hatua mbalimbali za kisheria.

Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya

Katika misako dhidi ya dawa za kulevya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha lilikamata watuhumiwa 26 wakiwa na kilogramu 196.4 za mirungi, na watuhumiwa 22 wakiwa na kilogramu 32 za bangi. Aidha, hekari 10 za mashamba ya bangi ziliteketezwa. Watuhumiwa wote wa dawa za kulevya tayari wamefikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.

Mapambano Dhidi ya Ujangili

Kamanda Masejo pia ameeleza kuwa katika mapambano dhidi ya ujangili, watuhumiwa wawili walikamatwa wakiwa na kilogramu 20 za nyama ya nungunungu. Watuhumiwa hao tayari wamefikishwa mahakamani na kesi zao zinaendelea.

Ukamataji wa Pombe Haramu na Wizi

Katika operesheni hiyo, watuhumiwa 38 walikamatwa wakiwa na lita 172 za pombe haramu aina ya Moshi, pamoja na mitambo minne ya kutengeneza pombe hiyo. Wote wamefikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Aidha, jumla ya watuhumiwa 202 wa makosa ya wizi walikamatwa na kesi zao zinaendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limewahimiza wananchi kutojihusisha na vitendo vya uhalifu, huku likiwataka madereva wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali na madhara mengine.