Dk.Gwajima awajia juu wazazi waliowapiga watoto waliosema ukweli mahakamani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:36 PM Feb 19 2025
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.
Picha: Mtandao
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima.

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, amekemea vikali wazazi na walezi wanaowapiga watoto wanaosema ukweli mahakamani wakiwalazimisha kupotosha ili kuharibu kesi.

Kwa mujibu wa taarifa aliyoweka leo kwenye ukurasa wake wa Instagram, amesema Februari 18, mwaka huu alipokea taarifa kutoka kwa raia mwema na kuthibitisha kuwa mkoani Tanga, Wilaya ya Bumbuli, kuna kesi inaendelea dhidi ya watoto kadhaa wa Kata ya Dude B, Shule ya Msingi (Jina limehifadhiwa) ambao walifanyiwa ukatili wa kijinsia.

Amesema Febriari 16, mwaka huu, wakiwa mahakamani waliwataja watuhumiwa na baada ya hapo, mmoja hao aliporudi nyumbani alipigwa na kuumizwa vibaya mkononi kisa kwanini amesema ukweli, wakati walimwambia akane, asiseme ukweli.

“Nakemea vikali aliyempiga mtoto huyu , Kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, nimeelekeza aliyempiga mtoto huyo ashtakiwe polisi mara moja, ili hatua stahiki zichukuliwe na mtoto apatiwe huduma zote stahiki pia, yeye na watoto wengine manusura wa ukatili huo wapelekwe nyumba salama,”amesema Dk. gwajima.

Aidha, amesema Wiraza inaendelea kuchukua hatua kwa wote wanaowatisha watoto wasipate haki zao na kuomba jamii kuendelea kutoa taarifa kwenye ofisi za serikali na vituo vya polisi.