UKUMBI wa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu, maarufu Mahakama ya Mafisadi, umezizima na kutawaliwa vilio baada ya Jimmy Mlaki na mwenzake kutiwa hatiani na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine gramu 509.63.
Hukumu ya mahakama hiyo ilitolewa mbele ya Jaji Sedikia Kisanya baada ya mahakama kuona ushahidi wa upande wa Jamhuri ulithibitisha kosa dhidi ya washtakiwa bila kuacha shaka.
Mlaki, mkazi wa Kinondoni na Stanley Ngowi, mkazi wa Tabata, walishtakiwa kuwa Januari 27, 2020, maeneo ya Ubungo Kibo, mkoani Dar es Saalam, walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine gramu 509.63 ndani ya begi.
Upande wa Jamhuri katika shauri hilo uliita mashahidi wanane na vielelezo 14 na upande wa utetezi, uliita shahidi mmoja na washtakiwa walijitetea wenyewe.
Akisoma hukumu, Jaji Kisanya alisema wenye jukumu la kuthibitisha shtaka bila kuacha shaka yoyote ni Jamhuri, hivyo hoja iliyoko mbele ya mahakama ni endapo waliweza kuthibitisha kwa kiwango kinachotakiwa.
"Maswali ya kujiuliza ni je, unga uliodhaniwa ni heroine ulichukuliwa kwa washtakiwa, vilivyokuwamo ndani ya begi ni heroine, utunzaji vielelezo ulizingatia utaratibu na mwisho ukamataji kama ulifuata utaratibu pia," alisema Jaji Kisanya.
"Ushahidi unaonesha washtakiwa walitia saini, hakuna ushahidi wa saini za washtakiwa kughushiwa. Mahakama inawatia hatiani washtakiwa wote kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine gramu 509.63," alisema Jaji Kisanya.
Mahakama iliwaruhusu Mawakili wa Jamhuri na upande wa utetezi kuwasilisha hoja zao kabla ya kutoa adhabu. Wakili wa Serikali Mwandamizi Ellen Masululi alidai Jamhuri haina kumbukumbu ya makosa mengine ya jinai dhidi ya washtakiwa isipokuwa wanaomba wapewe adhabu kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala, akiwasilisha maombolezo dhidi ya washtakiwa, aliomba mahakama iangalie umri wa washtakiwa, ni vijana wadogo. Aliomba wapewe adhabu ya kujifunza badala ya kuwapoteza kabisa.
Akitoa uamuzi Jaji Kisanya alisema mahakama imezingatia hoja za pande zote mbili, lakini adhabu ni ileile iliyoainishwa kisheria, adhabu kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya ni kifungo cha maisha gerezani na hakuna adhabu ya chini.
"Iliwahi kutolewa adhabu ya chini na mahakama hii, kesi ilipokwenda mahakama ya juu ikaonekana mahakama hii ilikosea, ilitakiwa kutoa adhabu ya kifungo cha maisha," alisema.
Baada ya kusema hayo, Jaji Kisanya alisema washtakiwa wote wanahukumiwa kifungo cha maisha jela kama inavyoelekeza katika sheria na wanayo haki ya kukata rufani.
Mahakama hiyo pia iliamuru vielelezo ambavyo ni Vilio vyatawala kortini washtakiwa wakihukumiwa kifungo cha maisha. viteketezwe na simu zirudishwe kwa washtakiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED