JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe, limefanikiwa kumkamata mwanamume raia wa nchi jirani ya Malawi, kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali, ambazo ni meno ya tembo ya zaidi ya Sh. milioni 155.
Tukio hilo lilitokea jana, Februari 16, 2025 saa 4:30 usiku katika Kitongoji cha Msia, Kata ya Chitete, Wilaya ya Ileje, mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Februari 17, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augostino Senga, alisema mtuhumiwa huyo, Chisamba Siame Kameme (60), alikamatwa kupitia operesheni za kiintelijensia, misako na doria zinazoendelea kwa ushirikiano na Idara ya Wanyamapori Wilaya ya Ileje.
Kamanda Senga, alisema tathmini ya awali ya wataalamu imebaini kuwa meno hayo, vipande 18 vyenye uzito wa kilo 84.2 yana thamani ya shilingi 155,311,020 sawa na Dola 60,000 za Marekani.
Aidha, Kamanda Senga alifafanua kuwa, meno hayo yametokana na tembo watatu na thamani ya tembo mmoja inakadiriwa kuwa takribani Sh. milioni 51.7.
Alisema kwa sasa, mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi hilo, huku uchunguzi zaidi ukiendelea kabla ya kufikishwa mahakamani, kwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe, limewaonya vikali watu wanaojihusisha na ujangili wa wanyamapori na kuacha mara moja, likisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa, kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo haramu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED