Tanzania, UNODC kuimarisha ushirikiano kukabiliana na uhalifu wa mazingira

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:25 PM Feb 17 2025
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na Uhalifu, Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki (UNODC ROEA), imejipanga kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kudhibiti uhalifu unaoathiri mazingira (Enviromental Crimes) na kulinda bayoanuwai.

Hayo yamejiri leo Februari 17,2025 katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana na Mwakilishi wa Kanda wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya na Uhalifu, Ofisi ya Kanda ya Afrika Mashariki (UNODC ROEA), Ashita Mittal, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho, Chana amesema kupitia kikao hicho Wizara ya Maliasili na Utalii na UNODC wamepata fursa ya kuangalia jinsi UNODC inavyounga mkono jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kukabiliana na uhalifu unaoathiri mazingira, kuangazia miradi inayoendelea, ikiwa ni pamoja na usafirishaji haramu wa nyara na mazao ya misitu, uvuvi haramu na usalama wa baharini.

Pia, Chana ametumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa UNODC kwa msaada wa kifedha na kiufundi uliotolewa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kupambana na uhalifu unaovuka mipaka (Transnational Organized Crimes) ikiwemo Biashara Haramu ya Nyara(IWT) kupitia Kitengo cha Udhibiti wa pamoja kilichopo Bandari ya Dar es Salaam (Joint Port Control Unit – JPCU).

“Biashara Haramu ya Wanyamapori  sio tu inaleta tishio kwa usalama wa rasilimali za wanyamapori na misitu miongoni mwa nchi wanachama, hivyo kuathiri uchumi wetu na kuwezesha uhalifu mwingine wa kupangwa kama vile utakatishaji fedha na ugaidi” Chana amesisitiza.

Kwa upande wake, Ashita Mittal ameahidi kuwa UNODC itaendelea kushirikiana na  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mapambano dhidi ya uhalifu unaovuka mipaka kwa kutoa zaidi mafunzo katika nyanja mbalimbali na vitendea kazi kupitia programu mbalimbali zitakazoandaliwa na pande zote mbili.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Maafisa kutoka UNODC na Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

3