DC Bomboko abaini kiini mafuriko Mtakuja, aja na mwarobaini

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 12:04 PM Feb 20 2025
Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Hassan Bomboko.
Picha: Mtandao
Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Hassan Bomboko.

MKUU wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Hassan Bomboko, amekutana kwa zaidi ya saa tano na wakazi wa Kijiji cha Mtakuja kilichopo Kata ya KIA, kujadili na kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la mafuriko ya mvua, ambayo yamekuwa yakiathiri makazi ya watu kila mwaka, na ekari 306 za mazao ya nyanya, hoho, pilipili na nafaka, hasa mahindi na maharage.

Katika kutafuta kiini cha tatizo hilo, Bomboko na timu yake ya wataalamu kutoka Bonde la Mto Pangani (PBWO) na maofisa wa Wilaya ya Hai, wamebaini chanzo ni kujifukia kwa Mto Kikuletwa, unaotokea Simanjiro, mkoani Manyara na maji yanayokosa mwelekeo yakitokea Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, huku wakulima nao wakichepusha wenyewe maji ya mto huo kwenda kwenye mashamba yao. 

Akizungumza jana, baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na wakazi zaidi ya 6,000 walioko Mtakuja, Mkuu huyo wa Wilaya, amesema: 

“La kwanza hapa, ni kwamba mto umejifukia na hata ufanyaje maji yataenda kwenye mashamba. Bila kuufukua, hata uweke kalavati 100 zivushe maji pale, maji yanayotoka huko yaje hayatakuja. 

“Kwa hiyo la kwanza, tumeona mito umejifukia. La pili, tumetengeneza njia zisizo za asili kutoa maji katika mto. Kwa hiyo maji tu lazima yatatoka hapa yafuate zile njia za kutengnezwa na binadamu, kwa sababu mto umefukiwa. 

…Na hii ilikuwa pia hoja ya wenzenu wa Arumeru na Simanjiro; kwamba wakulima wamechepusha mto kupeleka kwenye mashamba yao. Ndio ukweli; yaani huu mto ulishakufa, halafu tukachepusha maji kutoka kwenye mto wa asili, tukapeleka kwenye mashamba, kupitishia mfereji namba 9 na mfereji mkuu.” 

Katika kikao hicho, Eliachi Laizer, Mkazi wa Kijiji cha Mtakuja, amemweleza Bomboko kuwa, Kijiji hicho ukiachilia mbali mafuriko, kinatishiwa na kero ya uvamizi wa tembo katika makazi ya watu na mashamba ya kilimo, ubovu wa miundimbinu ya barabara, kukosa mavuno ya chakula kwa miaka sita sasa, kukosekana kwa soko na uhaba wa watumishi wa kada ya afya katika Zahanati ya Mtakuja. 

“Kuna kero moja kubwa inatusumbua. Barabara zetu zinatesa sana na ninyi ni mashahidi, kwamba mmepitia barabara hii. Juzi kati hapa, kaugua mama mmoja homa kali ya kupelekwa hospitali, lakini kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mbaya pikipiki iliyombeba ilianguka na mama aliumia akiwa tayari amezidiwa. 

Zaidi aliongeza, “Serikali tunaomba mtusaidie kuboresha hii miundombinu ya barabara, ni mbovu na hazipikiti Mtakuja.Mwaka huu, watu hawajavuna kitu kutokana na tembo ambao wanakula mazao. Chonde chonde, serikali yetu mzichukue kero hizi mkazifanyie kazi wananchi hawa wapate kupona.”

Mariam Athuman, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Upareni, yeye amemweleza Bomboko kuwa, kwa miaka sita sasa wamekaa bila kuvuna chakula, kwa sababu ya mafuriko yanaua mazao. 

“Mwaka 2020, asilimia 75 watu nyumba zilianguka kutokana na mafuriko.Lakini mafuriko hayo yanatokana na miundombinu ya maji kule yanapotokea. Hakuna miundombinu ya maji, ambayo inaweza kuelekeza mafuriko hayo kuelekea kwenye mto.

“Mafuriko hayo yakifika pale kwenye kalavati ambako watu walienda kufanya kikao cha vijiji sita vinavyoathirika na mafuriko yanasambaa. Kwa hiyo yakisambaa yanakuja kutathiri sisi katika makazi yetu.” 

Awali, Diwani wa Kata ya KIA, Tehera Kipara, akizungumzia mafuriko hayo amesema: “Chanzo kabisa cha mto kuharibika ni pale kwenye lami. Pale pakiwekwa daraka kubwa maji yapite kwa utaratibu, maji yatatengeneza hata njia kurudi mtoni lakini ukweli ni kwamba maji hayapiti tena mtoni na wala hayafiki.

 …Maji yamekosa mwelekeo, hayaendi mtoni na yanakimbilia mashambani na kuua mazao ya wakulima.”

Akijibu kero za wananchi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Hai, Dionis Myinga, amesema tayari serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mtakuja, kitakachojengwa eneo hilo sambamba na Shule ya Sekondari ya Ufundi.