Waziri Mbarawa akagua ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Ibadakuli, Shinyanga

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 05:10 PM Feb 21 2025
Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa akiangalia mchoro wa ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Ndege Shinyanga.
Picha: Marco Maduhu
Waziri wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa akiangalia mchoro wa ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Ndege Shinyanga.

WAZIRI wa Uchukuzi Prof.Makame Mbarawa, ametembelea kukagua ujenzi Uwanja wa Ndege Ibadakuli Shinyanga, kusimamia maagizo ambayo yalitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kuwa uwanja huo hadi kufikia Aprili ufungwe Taa na ndege zianze kutua nyakati za usiku.

Mbarawa amefanya ziara hiyo jana kwa kuzungumza na wasimamizi wa ujenzi wa upanuzi wa uwanja huo wa Ndege,Wakandarasi, pamoja na kutembelea kuona ujenzi wa miundombinu yake.

Amesema ujenzi wa uwanja huo wa ndege baadhi ya miundombinu ambayo ni ya muhimu tayari imekamilika, ikiwamo barabara ya kutua na kurukia ndege (Runway),na kuwaagiza wasimamizi wa ujenzi wa uwanja huo na TANROADS,kuhakikisha wanamsimamia Mkandarasi aagize malighafi na kuzifunga Taa kwenye uwanja huo ili kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

“Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Februari 16 alipofika kwenye ujenzi wa uwanja wa Ndege Shinyanga, aliagiza ifikapo April Mosi, uwanja huu uwekewe Taa ili uanze kutumika nyakati za usiku, hivyo TANROADS hakikisheni Mkandarasi anaweka “Order ya Material”ili Taa hizo zifungwe na kutekelezwa kwa agizo la Waziri Mkuu,”amesema Prof.Mbarawa.

Aidha, amempongeza pia Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha jitihada zake za kuhakikisha ujenzi wa uwanja huo wa ndege unafanikiwa pamoja na viwanja vingine vitatu kikiwamo cha Sumbawaga,Tabora na Kigoma,na kwamba haikuwa kazi rahisi, lakini sasa hivi viwanja hivyo vina kwenda kukamilika na kutoa huduma ya usafiri wa Anga kwa wananchi. 

Amewapongeza pia Wakandarasi kwa uvumilivu wao, kwamba ujenzi wa upanuzi wa uwanja huo wa Ndege Shinyanga ulisainiwa mwaka 2017, lakini katikati ukasuasua, ndipo Rais Samia akasimama kidete ili ujengwe, na ujenzi wake Rasmi ukaanza mwaka 2023, na mpaka sasa wameendelea nao na wapo hatua za mwisho kuukamilisha.

Mwakilishi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Lugano Mwinuka, amesema uwanja huo wa Ndege wa Shinyanga, zitakuwa zikitua ndege za masafa ya karibu zenye uwezo wa kubeba abiria 70-76 pamoja na kutumika kama dharura na utakuwa”feeder airport”.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amemshukuru Rais Samia juu ya ujenzi wa uwanja huo wa Ndege, kwamba amefungua fursa za kiuchumi mkoani humo.

Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Donatus Binamungu, amesema ujenzi wa upanuzi wa uwanja huo wa ndege Shinyanga umefikia asilimia 74, na kwamba barabara ya kutua ndege imekamilika kwa asilimia 100 na ndege zinaweza kutua mchana, na kueleza watamsimamia Mkandarasi kuagiza Taa ili zifungwe na kuanza kutumika nyakati za usiku hadi ifikapo mwezi Aprili.