Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imesema kumekuwa na ongezeko kubwa la wananchi wanaotoa notisi za kuishtaki serikali, ambapo idadi imefikia zaidi ya 500 kwa mwaka. Hali hii inaonesha kuwa baadhi ya viongozi na watumishi wa umma wanakiuka misingi ya utawala wa sheria.
Akizungumza leo, Februari 17, 2025, katika uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria na Kliniki ya Sheria bila Malipo, Mkurugenzi wa Huduma za Uratibu na Ushauri wa Kisheria, Neema Ringo, ambaye ni mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema ongezeko hilo linadhihirisha kuwa wananchi wengi wanakwazwa na namna wanavyohudumiwa na viongozi au watumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao.
"Ongezeko hili linaonesha kuwa kuna maeneo ambayo viongozi na watendaji wa serikali hawazingatii utawala wa sheria au hawatoi mwongozo wa kutosha kwa wananchi kuhusu taratibu za kufuata. Hii inawafanya wananchi kuhisi haki zao zinakiukwa, na kwa kweli, baadhi yao wanakuwa na madai ya msingi, hivyo kutoa notisi za kuishtaki serikali," amesema Ringo.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali imeanzisha kamati hizo za ushauri wa kisheria ambazo zitasimamiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na ofisi za Wakuu wa Wilaya na Mikoa. Kamati hizo zitakuwa kiunganishi kati ya wananchi na serikali kwa lengo la kusikiliza malalamiko na kutoa ushauri wa kisheria kabla ya wananchi kufikia hatua ya kufungua mashitaka mahakamani.
"Kamati hizi zitatoa fursa kwa wananchi kueleza changamoto zao na kupata mwongozo wa kisheria kwa wakati, kabla ya kufikia hatua ya kuishtaki serikali. Pia zitawasaidia wananchi kuelewa taratibu za kisheria ili wasipoteze haki zao kwa kuchelewa kuchukua hatua stahiki," ameongeza Ringo.
"Suala hili si jukumu la Mkuu wa Mkoa pekee au Mkuu wa Wilaya, bali litashughulikiwa na wataalamu wa kisheria. Wataalamu hawa watatoa ushauri wa kitaalamu kwa wananchi kuhusu taratibu wanazopaswa kufuata ili matatizo yao ya kisheria yapatiwe ufumbuzi kwa njia sahihi," amesema Mtanda.
Aidha, Mtanda ameeleza kuwa mashitaka mengi dhidi ya serikali hutokana na maamuzi yanayofanywa na viongozi bila kuzingatia usawa, ambapo baadhi ya wananchi wanahisi haki zao zinapuuzwa.
"Mashtaka mengi dhidi ya serikali yanatokana na maamuzi tunayofanya sisi viongozi, hasa pale tunapoyashughulikia madai ya wananchi kwa misingi ya huruma badala ya sheria, au kwa kuegemea upande mmoja," amefafanua.
Pia amesisitiza kuwa kamati hizo zitakuwa msaada mkubwa katika kushughulikia masuala ya ushauri wa kitaalamu kuhusu mikataba mbalimbali. Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na kamati hizo ili kurahisisha michakato ya kisheria, badala ya kutegemea ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pekee, jambo ambalo mara nyingi husababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa mikataba.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED