Kitabu cha JUA Na UA, ambacho ni sehemu ya mfululizo wa vitabu vya hadithi za watoto vilivyoandikwa na Mtanzania Prudence Zoe Glorious, kimezinduliwa rasmi mwishoni mwa wiki, Februari 15, 2025.
JUA Na UA ni kitabu kinachobeba falsafa za Kitanzania, kilizinduliwa katika ofisi mpya ya PZG-PR, iliyopo 50 Msasani Road, Oysterbay, Dar es Salaam kikiwa na lengo la kukuza fikra za watoto, kuchochea ubunifu wao, na kuwajengea uelewa wa hekima iliyomo katika urithi wa utamaduni wa Tanzania. Kitabu hiko kinatarajiwa kuwa mkusanyiko wa hadithi zinazovutia na kufundisha maadili muhimu kwa watoto, huku kikichochea ari ya ubunifu na kuwaimarisha katika uhusiano wao, asili yao, na maadili ya Kiafrika.
Katika kitabu hiko, kuna wahusika wawili wakuu: JUA, anayewakilisha mtoto wa kiume wa Kiafrika, na UA, anayewakilisha mtoto wa kike wa Kiafrika. Watoto hawa wawili wanalelewa katika familia ya Kitanzania inayozingatia maadili na desturi za Kiafrika.
Kitabu JUA na UA kina jumla ya kurasa 24, zenye simulizi mbalimbali zinazoelimisha watoto kuhusu maadili. Baadhi ya maudhui yaliyomo ni:
Kupitia maudhui hayo, kitabu hiko kinaonyesha maisha ya watoto wa Kitanzania na Kiafrika katika familia zao na jinsi wanavyotumia muda wao nje ya shule, hasa wakati wa likizo au mwishoni mwa wiki.
JUA na UA kinasisitiza umuhimu wa wazazi kutumia muda na watoto wao kwa kutembelea mbuga za wanyama ili kuwaona wanyama kama tumbili wakiruka kutoka mti mmoja hadi mwingine kwa mikono yao mirefu, simba wakiunguruma na kutembea kwa madaha kwenye nyasi za rangi ya kahawia, pundamilia wakijivunia mistari yao ya kipekee, lakini zaidi ya yote, twiga—wanyama wenye mwendo wa upole na wa madaha.
Uzinduzi wa kitabu hiko katika ofisi mpya ya PZG-PR uliwapa fursa wageni waalikwa kuzungumza na mwandishi, Prudence Zoe Glorious, ambaye alisimulia safari yake ya ubunifu na umuhimu wa kuandika kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho. Prudence, ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa PZG-PR, alithibitisha dhamira yake ya kukuza fikra na ubunifu wa watoto wa Kitanzania kupitia usomaji wa vitabu, jambo lililomfanya kuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika sekta ya fasihi na mahusiano ya umma.
"Nilitamani kuandika kazi ya fasihi yenye wahusika wakuu watoto wa Kiafrika, ili iwe kioo chanya cha Uafrika kwa kuunganisha falsafa zetu na urithi wetu katika hadithi tunazowasimulia watoto wetu. JUA Na UA ni kielelezo cha utamaduni wa Tanzania, kinachohamasisha watoto kufikiri kwa kina, kujivunia utamaduni wao, na kuendeleza uwezo wao wa ubunifu. Pia, kinachochea fikra, na kama tunavyojua, ubunifu ni kiwango cha juu kabisa cha akili," alisema.
Hafla hiyo pia ilihusisha maonyesho ya stadi za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati (STEM) kwa watoto, burudani, na fursa ya kununua nakala za vitabu vilivyosainiwa, jambo lililowafanya watoto, wazazi, familia, na wapenda fasihi kwa ujumla kufurahia tukio hilo la kihistoria.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED