Watanzania wametakiwa kuepuka mashinikizo yoyote yanayoweza kuhatarisha usalama wa nchi, yakiwemo maandamano, hasa wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Rai hiyo imetolewa na Nabii wa Kanisa la Heavenly Image Manifest (HIM), Nabii Edmund Mystic, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu mkesha mkubwa wa kuliombea Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan, na uchaguzi mkuu ujao.
Mkesha huo unatarajiwa kufanyika Februari 28, mwaka huu, katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, ukihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa.
"Tumeona mwaka jana jinsi hali ilivyokuwa nchini Kenya baada ya machafuko kutokea. Watumishi wa Mungu walihubiri kuhusu hatari hizo, lakini wengi hawakuzingatia. Sisi kama Watanzania, tunapaswa kutambua kuwa usalama wa Taifa letu ni jukumu la kila mmoja wetu. Ni muhimu kuepuka shinikizo lolote linaloweza kuleta machafuko na sisi viongozi wa dini tunapaswa kusimama imara kuliombea Taifa," alisisitiza Nabii Edmund.
Aidha, amewataka wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu kuepuka kutegemea waganga wa kienyeji, akisisitiza kuwa maandiko ya Biblia yanaeleza wazi kuwa "amelaaniwa mtu anayemtegemea mwanadamu."
"Wanasiasa wengi hawafahamu kuwa mganga wa kienyeji anaweza kumsaidia mtu kushinda uchaguzi kwa kutumia nguvu za kiroho zinazotokana na madhabahu zisizo za Mungu. Hili ni jambo la hatari, na wagombea wanapaswa kumtegemea Mungu badala ya mbinu hizo," alisema.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa wagombea wote kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na kwa mujibu wa sheria zilizowekwa nchini.
"Tufike mahali ambapo tunakuwa na uchaguzi ulionyooka, huru, na wa haki. Kiongozi anayepaswa kushinda ni yule ambaye Mungu amemkusudia kushika nafasi hiyo," alisisitiza Nabii Edmund.
Kuhusu mkesha wa maombi, alisema kuwa kanisa lina jukumu kubwa la kulibeba Taifa kwa maombi, na kupitia mkesha huo, wataomba kwa ajili ya Taifa na kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan, kwani yeye ndiye mtawala wa sasa na amebeba hatima ya Watanzania wengi.
"Hatuwezi kuombea serikali ijayo pasipo kuanza na serikali iliyopo madarakani. Ni muhimu kumwombea Rais Samia ambaye Mungu amemuweka kwenye nafasi ya uongozi," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED