Biteko: EWURA mmeleta utulivu kwenye nishati

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:07 PM Feb 17 2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Mashaka Biteko.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Mashaka Biteko.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Mashaka Biteko, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa usimamizi thabiti wa huduma za nishati na maji nchini ambao ameeleza kuwa umechangia kuleta na kuimarisha utulivu kwenye sekta ya nishati na taifa kwa ujumla.

Biteko ametoa pongezi hizo leo Februari 17, 2025  wakati akifungua kikao cha nne cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa EWURA kinachofanyika jijini Tanga.

"EWURA mnafanya kazi kubwa ya kudhibiti upatikanaji wa huduma za uhakika za umeme na mafuta nchini kwa ufanisi mkubwa, mmeleta utulivu kwenye sekta ya nishati nchini, mmerahisiha mazingira ya uwekezaji kwenye CNG, vituo vya mafuta vijijini na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwenye nishati safi ya kupikia, nawapongeza sana." amesema Biteko.

Dk. Biteko amesisitiza EWURA kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kiudhibiti kuhusu ajenda ya misheni 300 ya umeme  na kuwasimamia watoa huduma wanaodhibitiwa kuhakikisha wanakuwa na mikataba ya huduma kwa mteja inayotekelezeka.

Aidha, ameitaka EWURA kuhakikisha inaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara ya mafuta nchini, na kushirikisha wadau  na watoa huduma wanaodhibitiwa kwenye maamuzi ya kiudhibiti ili utekelezaji wake uwe na tija.