Tanzania yaalika wawekezaji Sekta ya Nishati mkutano Wiki ya Nishati Afrika

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 01:50 PM Nov 07 2024
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi, Dk. James Mataragio akiwasilisha kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati Tanzania wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika unaofanyika Cape Town Afrika ya Kusini.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi, Dk. James Mataragio akiwasilisha kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati Tanzania wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika unaofanyika Cape Town Afrika ya Kusini.

WIZARA ya Nishati imetumia jukwaa la Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika unaofanyika Cape Town Afrika Kusini, kueleza fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya nishati.

Kadhalika, imetumia jukwaa hilo, Tanzania na kukaribisha wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hiyo Tanzania.

Tukio hilo lilifanyika juzi kupitia wasilisho la Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo, anayeshughulikia mafuta na gesi, Dk. James Mataragio, aliyebainisha fursa katika maeneo mbalimbali ikiwamo uwekezaji katika vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, miundombinu ya mafuta na gesi, miradi ya nishati jadidifu na viwanda vya petrokemikali.

Katika eneo la vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, Dk. Mataragio alieleza kuwa tayari wizara imekamilisha maandalizi muhimu kuelekea tukio la uzinduzi wa duru ya tano ya kunadi vitalu hivyo vya mafuta na gesi asilia vilivyo wazi ambalo litazinduliwa rasmi Machi, 2025.

“Tunatarajia kunadi jumla ya vitalu 26 vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini. Kati ya vitalu hivyo, vitalu 23 vipo eneo la baharini na vitatu (3) vipo eneo la ziwa Tanganyika” alisema Dk.Mataragio.

Pia, alisema ipo fursa kwa wawekezaji kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuendeleza vitalu vya Eyasi-Wembere, Mnazi Bay Kaskazini na Songo Songo Magharibi, vitalu ambavyo Shirika hilo limeendelea kuvifanyia utafiti wa mafuta na gesi asilia. 

Kamishna wa Petroli na Gesi Wizara ya Nishati Goodluck Shirima (watatu kushoto), Kamishna Msaidizi wa Petroli Wizara ya Nishati Joyce Kisamo (wa nne kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa PURA Charles Sangweni na washiriki wengine waliohudhuria wakifuatilia wasilisho la fursa za uwekezaji nchini Tanzania. Wasilisho hilo lilifanywa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia masuala ya mafuta na gesi, Dk. James Mataragio wakati wa Mkutano wa Wiki ya Nishati Afrika unaofanyika Cape Town Afrika ya Kusini.
Katika wasilishohilo, Dk.Mataragio alisema data za vitalu vyote vitakavyopelekwa katika mnada na vile vinavyoendeshwa na TPDC, zinapatikana kwa ajili ya wawekezaji kuona na kununua na kwamba miongoni mwa aina za data hizo pamoja na nguvu sumaku ya miamba, uzito wa miamba, mitetemo na visima. 

Maeneo mengine ya uwekezaji aliyoyataja katika sekta ndogo ya mfatuta na gesi asilia ni uwekezaji katika ujenzi wa vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari na viwanda vya petrokemikali kwa kutumia gesi asilia. 

Dk. Mataragio alieleza kuwa serikali imefanya kazi kubwa kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini na kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwamo Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP), na kwamba Tanzania ni sehemu sahihi kwa uwekezaji.