TAKUKURU yaanza kumulika Uchaguzi Mkuu 2025

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 09:09 AM Dec 26 2024
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo.
Picha:Mtandao
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya imesema itafuatilia mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu wa 2025, ili kudhibiti vitendo vya rushwa na kuhakikisha wanapatikana viongozi wanaostahili.

Aidha, imeviomba vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla kutoa taarifa pale watakapoona viashiria vya rushwa kwenye maeneo yao ili vidhibitiwe mapema kabla havijasababisha madhara kwenye mchakato huo.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya, Maghela Ndimbo alisema hayo kwenye kikao na viongozi wa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kilicholenga kufanya tathmini ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mikakati ya uchaguzi mkuu ujao.

Ndimbo alisema katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, taasisi hiyo haikupokea kesi yoyote ya rushwa wala taarifa za vitendo hivyo kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo na hivyo wanajipanga zaidi kudhibiti vitendo hivyo uchaguzi ujao.

“Pamoja na kampeni yetu ya ‘Takukuru rafiki’, tunahitaji ushirikiano wa pamoja na wadau ikiwamo vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla ili tuweze kufikia malengo yetu ya kutokomeza vitendo vya rushwa,” alisema Ndimbo. 

Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mbeya, Hamad  Mbeyale alisema ili kumaliza vitendo vya  rushwa TAKUKURU inapaswa kuendelea kutoa elimu juu ya haki pamoja na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa kwa wanaobainika kujihusisha na vitendi hivyo.

Alisema rushwa imekuwa ikisababisha haki za watu kupotelea mikononi mwa wasiostahili haki hiyo na hivyo kusababisha demokrasia kuharibika ndani ya nchi.

Mwenyekiti wa Chama cha ADC, Godfrey Davis alisema elimu ya rushwa inapaswa kuanzia ngazi za shule za msingi ili kutengeneza taifa lenye uzalendo na maadili akieleza kuwa wanayo matumaini na chombo hicho katika utekelezaji wa majukumu yake. 

Naye Mwenyekiti wa Maimamu na mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) mkoani Mbeya Sheikh Idd Tua alisema rushwa imelaaniwa katika vitabu tukufu na kwamba wanaofanya vitendi hivyo wanakiuka maandiko takatifu, hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.