UNAPOTAJA ugonjwa selimundu, tafsiri ya awali inayobeba picha halisi ni mateso kimwili, kiuchumi na kijamii.
Kuna safari zisizoisha hospitalini, kulala wodini, mahitaji ya kuongezwa damu mara kwa mara, huku upande wa pili ukiakisi gharama kwa anayemhudumia mgonjwa.
Hali ilivyo, sehemu kubwa ya wanaougua na kuuguza, uelewa wao kuhusu maradhi hayo ni mdogo; mara nyingi huufahamu undani wake pindi wanapokuwa katika pilika za matibabu. Vilevile, vituo vya tiba ngazi ya chini, katika itifaki ya utendaji, havina mamlaka ya kutibu shida hiyo.
Kuna cha simanzi zaidi; serikali inakiri nusu ya wanaozaliwa na selimundu hufariki dunia ndani ya miaka mitano baada ya kuzaliwa.
Ili kukabili ugonjwa huo, serikali italazimika kutenga Sh. bilioni 770 kutibu zaidi ya watoto 14,000 wanaozaliwa na maradhi hayo nchini kila mwaka.
Lakini haya yote yanaweza kuepukika ikiwa elimu itatolewa kwa wananchi kuhusu ugonjwa huu au kuwa na sheria inayozuia kuoana pasi na kupimwa selimundu.
Wataalamu wa selimundu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando jijini Mwanza na Hospitali ya Rufani ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma wamezungumza kwa kina na Nipashe kuhusu ugonjwa huu, hata kutoa ushauri huo kwa serikali.
Ili kutibu selimundu, tiba pekee ni kupandikiza uloto. Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, gharama ya matibabu hayo nchini inaanzia Sh. milioni 50 hadi 55 kwa kila mgonjwa. Upandikizaji uloto nchini kwa sasa unafanywa BMH kwa gharama za serikali.
Kwa watoto 14,000 wanaozaliwa na tatizo hili, maana yake serikali italazimika kutenga zaidi ya Sh. bilioni 770 kuwatibu watoto hao kila mwaka.
Daktari Bigwa wa Magojwa ya Watoto na Mtaalamu wa Selimundu katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando, Emmanuela Ambrose, anasema tatizo la ugonjwa huo ni kubwa nchini.
Bingwa huyo anasema utafiti unaonesha asilimia 75 ya watoto wanaozaliwa na ugonjwa wa selimundu duniani wanatoka Afrika. Tanzania ni nchi ya nne duniani na ya tatu Afrika kwa tatizo hilo. Wengi wao wanatoka Ukanda wa Ziwa Victoria.
Dk. Emmanuela anasema Bugando hivi sasa ina zaidi ya watoto 1,000 wenye shida ya selimundu wanaohudhuria kliniki kwa mwaka. Kila Jumatatu wanawaona watoto 30 hadi 50, huku Ijumaa wakiwaona watoto 50 hadi 80.
"Tunatoa ushauri na kuwaelimisha wazazi na walezi kuwa ugonjwa wa selimundu hurithiwa kutoka kwa wazazi wote wawili; baba na mama. Pia tunatoa elimu jinsi ya kuepuka kupata mtoto mwenye tatizo hili.
"Watoto wengi wanazaliwa wakiwa na shida hii. Tatizo hili ni kubwa kwa sasa kutokana na watu kutokuelewa wamerithi chembechembe za ugonjwa huu, wanatambua tu pale wanapopata mtoto mwenye shida hii.
"Kusubiri mpaka upate mtoto ni kuchelewa, wanapaswa watambue hali zao kabla ya kubeba ujauzito. Kama wote wana urithi wa selimundu, wafanye uamuzi mapema. Hivyo ni vyema wakapima kabla ya kuingia katika ndoa," Dk. Emmanuela anasema.
Bingwa huyo anashauri mtoto akishazaliwa tu apimwe. Akibainika ana tatizo hilo, aanzishiwe kliniki na matibabu ya selimundu mapema ambayo yatamsaidia kutibu matatizo yote yanayotokana na ugonjwa huo, hata kumfanya aishi muda mrefu.
Njia nyingine ya kukabiliana na ugonjwa huo, Dk. Emmanuela anashauri mama mjamzito anapoanza kliniki apimwe hali yake.
"Kama akibainika amebeba chembechembe za selimundu, iandikwe kwenye kadi yake ya kliniki "AS" (ana chembechembe za selimundu), iandikwe "SS" kama ana selimundu au "AA" kama hana chembechembe wala selimundu.
"Watoto wote watakaozaliwa na mama mwenye "SS" au "AS", lazima wapimwe hali zao watakapozaliwa. Hiyo itasaidia kuondokana na ugonjwa huu," Dk. Emmanuela anashauri.
Bingwa huyo pia anashauri shuleni kuwe na somo mahususi la selimundu kuchochea jitihada za kukabili ugonjwa huo na upimaji selimundu ufanyike hadi shuleni ili watoto wajue hali zao wakiwa wadogo, akiamini hatua hiyo itawasaidia kutambua hatari iliyoko mbele yao na watakuwa makini.
Dk. Emmanuela ana angalizo kwa jamii, akisisitiza kuwa matibabu ya selimundu ni ghali. Ni ugonjwa wa kudumu. Mzazi lazima awe na fedha.
Kuhusu matibabu ya selimundu, Bingwa wa Magonjwa ya Watoto MNH, Dk. Evance Godfrey, anafafanua kuwa mtoto akigundulika ana ugonjwa huo, anaanzishiwa dozi ya Folic Acid inayosaidia uzalishaji damu.
"Pia anaanzishiwa dozi nyingine ya Penicillin V inayozuia magonjwa yanayosababisha vifo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na anapofikisha umri wa miezi tisa anaanza dozi ya Hydroxyurea," Dk. Godrefy anafafanua.
Katika hilo la matibabu, bingwa mwenzake Dk. Emmanuela anatamani serikali isaidie kutoa dawa kwa wagonjwa wa selimundu, hasa dozi ya Hydroxyurea inayosaidia kupunguza shida zinazotokana na selimundu yakiwamo maumivu ya viungo, kulazwa hospitalini na kuongezwa damu mara kwa mara, kuzuia kupata kiharusi (kupooza) na damu kuwa nyepesi.
"Kupandikiza uloto ndiyo tiba ya selimundu, lakini ni gharama sana. Pia lazima uloto huo ni lazima utoke kwa ndugu yako unayeendana naye kibaiolojia (vinasaba). Hapa nchini ni watoto wanane tu wamefanyiwa upandikizaji na wote wako salama, lakini nina imani wengi zaidi watafanyiwa, hasa ambao Hydroxyurea haijawa msaada kwao," anafafanua.
KULIKONI KANDA YA ZIWA?
Dk. Emmanuela anasema Kanda ya Ziwa ni moja ya kanda za kitropiki ambazo zina tatizo kubwa la malaria, akiwa na ufafanuzi kwamba mwili wa binadamu umeshabuni njia ya kupambana na malaria kwa kusababisha hitilafu katika vinasaba na kuleta urithi wa selimundu.
"Kwa hitilafu hii warithi waliweza kuishi kwa kujikinga na ugonjwa wa malaria uliokuwa chanzo kikubwa cha vifo. Hitilafu hiyo ikirithiwa kutoka kwa wazazi wote wawili, ndiyo huleta ugonjwa wa selimundu.
"Kuoana wenyewe kwa wenyewe katika ukanda huu wa kitropiki linaonekana jambo la kawaida, lakini ni chanzo cha ongezeko la ukubwa wa tatizo la selimundu Kanda ya Ziwa.
"Kitu cha muhimu ni kufanya vipimo kabla ya kuoana na ikibainika mna urithi wa selimundu, bora msioane ili kuepuka kupata mtoto mwenye ugonjwa huu," anasema Dk. Emmanuela na kushauri kwamba, "ikiwezekana kuwe na sheria inayolazimisha wananchi kupima selimundu kabla ya kuoana.
Hoja ya kuepuka kuoana wenye urithi wa selimundu, inaungwa mkono na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu na Kansa kwa Watoto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Shakilu Jumanne, anayesema kuwa licha ya mikakati mingi ya kupunguza makali ya ugonjwa huo, hali ni mbaya nchini.
Dk. Jumanne anasema watoto wengi wanaendelea kuteseka na ugonjwa huo kutokana na uelewa mdogo wa wazazi kuhusu namna ya kuepuka mazingira yanayoweza kuchochea seli nyekundu kubadilika umbo na kuwa mundu.
Kama ilivyotolewa angalizo na mtangulizi wake Dk. Emmanuela, Bingwa Jumanne anashauri watu wenye vinasaba vya ugonjwa huo wasioane.
"Kila mwaka nchini, zaidi ya watoto 14,000 huzaliwa na ugonjwa huu. Kati yao, 10,000 huzaliwa mikoa ya Kanda ya Ziwa. Mwanza pekee wanazaliwa zaidi ya watoto 1,700 kila mwaka wenye tatizo hili," Dk. Jumanne anabainisha.
Kwa lugha rahisi ya hisabati, takwimu hizo zina maana kwamba, kila siku watoto 39 wanazaliwa wakiwa na ugonjwa wa selimundu nchini. Kati yao, 28 (asilimia 72) huzaliwa mikoa ya Kanda ya Ziwa huku Mwanza pekee ikiwa na wastani wa watoto watano kwa siku.
Kuhusu matibabu ya ugonjwa huo, Dk. Jummanne anaungana na Dk. Emmanuela kwamba njia ya uhakika zaidi ni kupandikiza uloto kutoka kwa ndugu wa karibu kwenda kwa mtoto mwenye tatizo.
"Matibabu ya selimundu ni ghali, hususani katika kupandikiza uloto. Hivyo, ili kuepuka haya, lazima jamii ikubaliane kupima kabla ya ndoa ili kuwaepusha watoto wetu na maumivu wanayopitia watoto wenzao wenye maradhi ya selimundu," bingwa huyo anashauri.
MIKASA MITAANI
Isivyo bahati, wote walio mifano ya kujifunza ni kinamama walimu, maradhi ya selimundu yamewatia misukosuko kwa watoto wao.
Mwalimu Hollo Lumala (33), miaka 12 iliyopita alibahatika kupata mtoto wa kike, lakini mikasa ya selimundu ilimpokonya kichanga hicho.
Kwa ufupi, alijifungua mwezi Desemba 2012 na maisha ya malezi yalikuwa shwari hadi Julai 29, 2013, ghafla mtoto alipata homa kali, kidole mkononi kikavimba na alipofikishwa katika zahanati ya Masengwa, wilayani Shinyanga, akapewa maelekezo ya tahadhari kutoka kwa tabibu "huyu mtoto anaonekana ana upungufu wa damu, mpelekeni hospitali kubwa".
Alipofikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga siku hiyo hiyo, ikathibitishwa ni shida ya upungufu wa damu, lakini wakati wa mchakato kumwongeza damu, mtoto alipoteza maisha akiwa na miezi saba tu duniani.
Mnamo Julai ya mwaka uliofuta, akiwa mkoani Dar es Salaam yaliko makazi yake, alijifungua mtoto wa kike baada ya kupitia mchakato wa uzazi ndani ya mwaka huo mmoja; mtoto akiwa salama kiafya hadi sasa.
Januari ya mwaka huu unaoisha leo, alibahatika kupata mtoto wa kiume. Safari hii mkasa ulianzia alikozaliwa hospitalini Kairuki, akagundulika ana manjano, hata ikamweka wodini kwa siku saba.
Mwalimu Hollo anasimulia maendeleo ya afya baada ya hapo yalikuwa mazuri hadi Julai mtoto alipogundulika kuvimba kidole cha mkono wa kulia. Aliwahishwa katika zahanati jirani alikopata huduma ya sindano ya kutoa sumu, ikihisiwa alikuwa ameng'atwa na mdudu.
Anasimulia kuwa baada ya siku tatu, kidole kingine cha mkono tofauti kilivimba. Mtoto akapelekwa katika Hospitali ya Kairuki, ambako huduma za kibingwa zikabaini ana selimundu.
Mwalimu Hollo anaeleza kuwa hatua ya kwanza ya tiba ilikuwa ni kukabili athari zinginezo, huku akiongezwa damu chupa moja, ikiendana na kuanzishiwa dozi ya tiba ya selimundu kwa mtoto mwenye umri wa chini ya miezi tisa.
Mwezi uliofuata, huku mtoto huyo akianza kuota meno, mama yake anasimulia aliona tena dalili za upungufu wa damu kwa mwanawe ambazo alikuwa ameshafundishwa hospitalini, hata akamrejesha alikotibiwa. Huko ikathibitishwa tena ana upungufu wa damu na akaongezwa, ikiendana na dawa.
Anasimulia kuwa mwezi Septemba alisafiri na mwanawe kwenda mkoani Shinyanga, mtoto akapatwa na dalili za awali, safari hii akalazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga kwa siku mbili, akiongezwa damu.
Kufika Novemba, Mwalimu Hollo anasimulia mkasa ukamrejea tena mwanawe, wakiwa Dar es Salaam, hata wakalazimika kufunga safari ya saa saba usiku kwenda Muhimbili ambako mtoto alipokewa na kulazwa kwa siku nne, akiongezwa damu chupa mbili.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, safari hii tiba iliendana na kuanzishiwa rasmi dozi ya Hydroxyurea inayozuia uwezekano wa maradhi mengineyo kama vile kiharusi, damu kuwa nyepesi na maumivu ya viungo yasiyokoma.
Mwalimu wa pili, Aman Stanslaus (37), mkazi wa Busega mkoani Simiyu, ukimwangalia kiumri na nyakati alizopitia, anashabihiana na mtangulizi wake, wote wakiangukia taaluma moja.
Miaka 10 iliyopita, alipoteza wanawe wawili kutokana na selimundu huku akitengana na mumewe. Katika miaka minne ya mwanzo ya ndoa na mwalimu mwenzake (jina tunalihifadhi), walipata mtoto.
Ilipotimu mwaka 2018, kukaripotiwa malalamiko ya mtoto wao anasumbuliwa na maumivu ya viungo vya mwili, wakati mtoto huyo akisoma shule ya bweni na kuanza matibabu.
Mwalimu Aman anawasilisha simulizi hiyo kwa sauti ya chini, inayobeba tafsiri ya simanzi, akiwa na ufafanuzi kwamba: "Baada ya vipimo katika Hospitali ya Wilaya ya Magu, madaktari walituambia kuwa mwanangu anasumbuliwa na homa.
"Baada ya muda akawa ameishiwa damu, wakamwongeza. Tukaruhusiwa kurejea nyumbani, lakini baadaye akaishiwa damu tena, ndipo madaktari wa hospitali hiyo walipojiuliza 'kwanini anaishiwa damu kwa muda mfupi baada ya kuongezwa?'
"Wakalazimika kumpima sikoseli (selimundu) na majibu yalipotoka alibainika kuwa 'positive' (taarifa chanya, yaani alikuwa na ugonjwa huo).
"Sikuwa na uelewa wa ugonjwa huu, lakini mtoto alianza kupatiwa matibabu na alirejea shuleni. Ghafla hali ilibadilika na kuishiwa damu."
Mwalimu Aman anataja ndiyo ukawa mwanzo wa kutokuelewana ndani ya familia, kila mmoja akimtupia lawama mwenzake kuwa chanzo cha tatizo. Baadaye lawama zote zilielekezwa kwake
"Hapo ndipo matibabu yakahamia kwenye miti shamba, lakini mimi sikuwa na mrengo huo. Mume wangu na familia yake walijikita katika imani hiyo. Mimi nikajikita katika huduma za hospitalini ingawa kuna wakati walimleta mganga wa kienyeji nyumbani kwa ajili ya kutoa huduma kwa mtoto," anasimulia.
Anasema kuwa wakati wanaendelea na matibabu ya mtoto huyo, alijifungua mtoto mwingine. Naye akawa na selimundu. Wakamwanzishia kliniki ya matibabu ya ugonjwa huo katika Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando.
"Baadaye nikapata mimba nyingine ya mtoto wa tatu. Wa kwanza aliendelea kusumbua na vurugu ziliongezeka nyumbani, maelewano yakatoweka. Mume wangu aliungana na familia yake na kusema mimi ni chanzo na hawakuamini kwamba ni sikoseli. Walidai ni 'chango' (ugonjwa unaowapata watoto unaofanana na degedege).
"Baadaye mtoto wa kwanza akapatwa na degedege. Nilikwenda naye Bugando, nilikaa naye kwa muda wa siku saba, wakamfanyia vipimo ikaonekana figo imeharibika sana kutokana na matumizi holela ya zile dawa za kienyeji. Ikawa ndiyo safari yake ya mwisho duniani... alipoteza maisha.
"Wakati huyo mwanangu akiwa mahututi hospitalini, yule wa pili aliomba kwenda hospitalini kumwona ndugu yake, kipindi hicho naye alikuwa anatibiwa nyumbani kwa miti shamba, wakamkatalia. Alilia hadi akapoteza fahamu. Akalazwa katika kituo cha afya kilichoko maeneo hayo, lakini alipozidiwa tukalazimika naye kumpeleka Bugando.
"Hapo nikawa na watu wawili; mmoja mochwari mwingine chumba cha wagonjwa mahututi, kwa wakati mmoja. Nilikwenda kuzika na baadaye nikarudi kumwuguza huyu mwingine. Hapo familia hatuelewani kabisa.
"Niliamua kuomba uhamisho ili niwe karibu na hospitali hii kwa ajili ya matibabu ya mtoto ambaye alikata kauli tangu kipindi kile akihitaji kumwona ndugu yake, ilimchukua miezi mitatu akiwa anakula kwa mpira. Miezi mitatu baada ya mwenzake kufariki (dunia) naye akaaga dunia... (simanzi inamtawala, anahamia kwenye kilio)."
Baada ya takriban dakika tano, mama huyo anaendelea na mazungumzo na mwandishi, akisimulia: "Baadaye nikajifungua mtoto wa nne. Daktari (wa Bugando) alinishauri niwapime watoto waliobaki hai. Majibu yalipotoka, mtoto wa tatu alionekana kuwa na sikoseli na wa mwisho alikuwa mzima kabisa.
"Daktari alishauri waanze kumshughulikia huyu mtoto wa tatu. Kipindi hicho nilikuwa ninalea mwenyewe. Tulitengana na baba yao kutokana na kunituhumu kwamba mimi ni chanzo kwa vyote vilivyotokea. Alitoa kauli kali kwamba 'heri watoto hao wamefariki dunia maana wamemgharimu kiuchumi," anadai Mwalimu Aman.
Mama huyo anasema anazingatia kliniki ya mwanawe huyo, akibainisha kuwa hakuwahi kufanya uchunguzi wa afya yake. Baada ya kupata matatizo hayo, alipima na majibu yalibainisha ana hali anayoiita "AS", ikiwa na tafsri ya kitabibu kwamba hana selimundu, lakini amebeba chembechembe za maradhi hayo.
Mwalimu Aman anashauri watu wanaoingia katika uhusiano wapime kwanza hali ya vinasaba vyao na kutokupendana kwa macho tu kwa kuwa athari itakayomkuta mtoto watakayemzaa ni kubwa na wakikaidi wakubaliane na matatizo watakayokutano nayo.
"Ninaomba serikali itoe elimu kwa jamii ili iwe na uelewa kuhusu ugonjwa huu kama magojwa mengine sambamba na kupunguza gharama za matibabu, hasa upandikizaji uloto pamoja na kuwa na wataalamu wa ugonjwa huu hadi ngazi ya vituo vya afya na zahanati," anashauri.
Binti wa mama huyo, Anthonia Bundala (10), anayeugua selimundu, mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Nundu, wilayani Ilemela, anaiambia Nipashe:
"Ninamshukuru sana Mungu, mama yangu, ndugu zangu na marafiki zangu shuleni, wananipenda sana. Ninapenda kusoma na mama ananisaida, nina imani ndoto yangu nitaifikia ya kuwasaidia watu wengine wenye ugonjwa kama wangu nitakapokuwa daktari."
MASHUJAA WA SELIMUNDU
Priscilla Chassam, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mashujaa wa Sikoseli Tanzania, anasema kuwa katika kutoa elimu ya ugonjwa huo wilayani Busega mwaka jana, walipimwa watu 365. Nusu yao (182) walikuwa na ugonjwa ya selimundu, wengine wana chembechembe za selimundu na wachache hawana chembechembe wala selimundu.
"Hapo utaona jinsi gani ugonjwa huo ulivyo mkali. Tunaendelea kutafuta fedha kuyafikia maeneo mengine ya vijijini," Priscilla anasema.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Selimundu Wizara ya Afya, Dk. Asteria Mpoto anabainisha kuwa serikali inafanya jitihada kuweka unafuu kwenye huduma za selimundu ikiwa ni pamoja na kuimarisha matibabu ya kibingwa ya upandikizaji uloto.
Anasema kuwa kwa kuanzia, serikali imegharamia matibabu ya kibingwa BMH kwa watoto wenye ugonjwa huo kwa kupandikiza uloto ili kuwapunguzia maumivu wanayoyapata.
Elisha John (12), mmoja wa watoto wanane walipona selimundu baada ya kupandikizwa uloto BMH, anasema: "Nilikuwa ninapata shida ya kuumwa kichwa, damu yangu ilikuwa inapungua mara kwa mara. Shuleni nilikuwa simalizi mwezi, lazima nitalazwa. Wiki nzima sihudhurii vipindi shuleni, tangu nimetibiwa sijasikia maumivu yoyote."
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, alisema zaidi ya watu 200,000 nchi wanaugua ugonjwa wa selimundu.
Alikuwa anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Hassan Toufiq aliyehoji idadi ya watanzania wenye selimundu na ni mikoa mingapi iliyoathiriwa zaidi na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Afya, Dk. Mollel, mikoa iliyoathiriwa zaidi na selimundu nchini ni Mwanza, Tabora, Kigoma, Mara, Dar es Salaam na Pwani.
"Utafiti unaonesha sehemu zenye maambukizi ya malaria kwa wingi, ndizo ambazo pia zina wagonjwa wengi wa selimundu," anasema Dk. Mollel na kubainisha kuwa Tanzania ina zaidi ya watu 200,000 wenye selimundu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED