RC Dendego apiga marufuku unywaji pombe nyakati za asubuhi

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 01:06 PM Apr 19 2024

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, akitoa maelekezo kwa watendaji ikiwemo kupiga marufuku kwa vijana kunywa pombe wakati wa asubuhi.
Picha: Thobias Mwanakatwe
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, akitoa maelekezo kwa watendaji ikiwemo kupiga marufuku kwa vijana kunywa pombe wakati wa asubuhi.

MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego,amepiga marufuku tabia ya wananchi kunywa pombe nyakati za asubuhi na kuagiza hali hii ikiendelea ataanza kuwachukulia hatua Watendaji wa kata ambao wanashindwa kukomesha vitendo hivyo.

Amepiga marufuku leo (April 19, 2024) wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kashamgu Halmashauri ya Itigi Wilaya ya Manyoni baada ya kukagua ujenzi wa zahanati ya kijiji ambapo alikuta baadhi wa wananchi katika kijiji hicho waking wa pombe saa 4:00 asubuhi wakati walistahili kuwepo mashambani kufanya kazi za uzalishaji.

"Sheria inasema siku za kawaida saa 10:00 jioni ndio muda wa kunywa pombe wewe Mtendaji wananchi wako asubuhi hii wanakunywa pombe na wewe upo unaona,mimi huwa sigombani na wananchi ndio staili yangu ya uongozi,nikikuta jambo linakwenda ndivyo sivyo nakamata mtendaji maana ana sheria kama za kwangu na ana mamlaka hayo,"amesema Dendego.

Dendego amesema ni lazima kuweka utaratibu kwenye vijiji haiwezekani nguvu kazi wanaanza kunywa pombe toka asubuhi halafu mwisho wa siku wananchi hao hao wanalalamika serikali haijaleta maendeleo.

"Mbaya zaidi nimekuta watoto wa kike ndo wanakunywa pombe,saa ngapi watoto wanaandaliwa kwenda shule,saa ngapi unasafisha nyumba,saa ngapi unaweka mazingira  ya mumeo kurudi nyumbani,sio sawa, akina mama mimi ni mkali kwenye maendeleo sitaki mambo ya hovyo,tunashindwa kulea familia sababu ya mambo haya ya hovyo, sasa watendaji wa vijiji,kata na tarafa sitaki kuona haya, Mwenyekiti wa kijiji kuna sheria ndogo zifanye kazi,"amesema Dendego