RC aagiza vikundi vyote huduma za fedha vijisajili

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:13 AM Jun 12 2024
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere.
Picha: Mpigapicha Wetu
MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere.

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere, ameelekeza watoa huduma ndogo za fedha mkoani mwake wasajili huduma zao za kifedha kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2018 na kutoa elimu kwa wateja wao kabla ya kuwakopesha.

Makongoro alitoa maagizo hayo jana wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Sumbawanga.

"Watoahuduma ndogo za fedha ni watu muhimu katika mkoa wetu wa Rukwa na taifa kwa ujumla. Pamoja na umuhimu huo, ninaagiza kuwa watoahuduma ndogo za fedha wote mkoani Rukwa wasajiliwe kwa mujibu wa sheria," alisema.

Makongoro alisema sambamba na zoezi la kusajili vikundi vidogo vya huduma ndogo za fedha, ni vyema pia kwa watoamikopo kutoa elimu kwa wanaowakopesha na kuwapa muda wa kuelewa mikataba kabla ya kuwapa mkopo.

"Mtoa huduma za kifedha toa elimu kwa yule unayetaka kumkopesha kuhusu huduma yako kabla ya kumkopesha. Na hili liende sambamba na wanaokopeshwa kupewa muda wa kutosha kusoma mikataba yao na kuielewa vizuri kabla ya kumkopesha, usimshtukize ule mkataba mpe muda ausome auelewe ndio umkopeshe," alisisitiza Makongoro.

Vilevile, aliagiza wakuu wa wilaya wote wa Mkoa wa Rukwa wahakikishe wanasimamia maelekezo yake kuanzia ngazi ya vijiji, kata, tarafa pamoja na halmashauri zote.

Mkuu wa Mkoa Makongoro Nyerere pia aliomba wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa kutoa ushirikiano ili kubaini watu wote wanaotoa huduma za fedha kinyume cha utaratibu wa kisheria ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Alishukuru wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa mkoa wake katika wilaya na halmashauri zake zote.