Rais Samia atoa pole Ubalozi wa Iran Nchini, kufuatia kifo cha Raisi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:38 PM May 25 2024
Rais Samia akiwa kwenye picha na Balozi wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran hapa nchini Hossein Alvandi Bahineh pamoja na Maafisa Mbalimbali wa Ubalozi huo.
Picha: Ubalozi wa Iran -Tanzania
Rais Samia akiwa kwenye picha na Balozi wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran hapa nchini Hossein Alvandi Bahineh pamoja na Maafisa Mbalimbali wa Ubalozi huo.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Mei 24, 2024 amewasili katika Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran hapa nchini na kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Rais wa nchi hiyo, hayati Ebrahim Raisi kilichotokana na ajali ya helikopta nchini Iran.

Baada ya kutoa rambirambi zake kwa kila afisa wa Iran aliyekuwepo ubalozini hapo, aliandika na kusaini kitabu cha kumbukumbu cha wahanga wa ajali ya helikopta nchini Iran. 

Katika ujumbe wake, aliandika, "Rambirambi zangu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na kifo cha ghafla cha Rais Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Amirabdollahian.

Tanzania inaungana na watu wa Iran katika kuomboleza na inaombea familia za wafiwa. Inna Lillahi wa Inna Ilayhi Rajiun. Samia Suluhu Hassan; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 24 Mei, 2024."

Hayati Raisi alifariki dunia Mei 19, 2024 mwaka huu kaskazini-magharibi mwa Iran, kwenye mteremko wa mlima katika eneo la Varzaghan, karibu na mpaka wa Azerbaijan Mashariki.

Wengine waliofariki katika ajali hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran, Hossein Amir-Abdollahian na maofisa wengine kadhaa.