MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Kaimu Mkeyenge, amesema hivi sasa wameelekeza nguvu kubwa kutoa elimu ya bima kwa wananchi, ili wajue faida ya kutumia huduma hiyo kujikinga na majanga au hasara.
Akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea maonyesho ya 48 ya biashara jijini Dar es Salaam, amesema huduma za bima zinayahusu maisha ya kila siku mtu kwa kuwa majanga hayapigi hodi.
“Tumebaini kwamba elimu ya bima kwa Watanzania iko chini sana, unakutana na mtu anakwambia bima ya nini. Bahati mbaya huwezi kuelewa umuhimu wake mpaka yakukute. Tunasema ni muhimu kuwa na bima kwa mali yako yoyote uliyonayo,” amesema.
Mkeyenge amewataka wawekezaji nchini kukata bima za biashara ili kuepuka hasara zitokanazo na majanga.
Amesema uwekezaji umeongezeka nchini hivyo ni muhimu wafanyabiashara na wamiliki wa kampuni kulinda mali zako kwa uhakika kwa kuzikatia bima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko na Mahusiano wa NIC, Karim Meshack, amewataka wakulima kuchangamkia bima ya kilimo na mifugo ili kutopata hasara wakati wa ukame, mafuriko au wizi wa mifugo.
Amesema wakulima wanaoweza kunufaika na bima ni wa pamba, korosho, kahawa, tumbaku, maharage, mahindi, mpunga, shayiri, alizeti na chai.
“Bima inamlinda mkulima dhidi ya ukame, mafuriko magonjwa/wadudu wasiodhibitika au kutibika, vimbunga na mvua ya mawe,” amesema.
Amefafanua kuwa lengo la kuweka bima kwa wakulima ni ili kuwakinga dhidi ya hasara baada ya majanga na kukuza uwekezaji.
Kuhusu mifugo amesema bima itamlinda mfugaji dhidi ya hasara itokanayo na vifo vya mifugo kwa ajali, wizi, magonjwa na uchinjwaji wa lazima kwa ushauri wa daktari.
Amesema mifugo inayolindwa ni ng’ombe wa maziwa, wa nyama, kuku na mbuzi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED