Mwalimu achanja mbuga wadai walipomvaa shuleni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:49 AM Apr 17 2024
Mwalimu awakimbia wanaomdai.
PICHA: MAKTABA
Mwalimu awakimbia wanaomdai.

WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Luwa katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, walikatisha masomo kwa takribani saa tatu baada ya wajasiliamali kufika shuleni hapo na kumfanyia shambulio la aibu Mwalimu Mkuu wa Shule kwa madai ya kushinikiza walipwe fedha wanazomdai mwalimu aliyekopa bidhaa kwao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Mwenyekiti wa Kijiji, Stedius Pastory, amesema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 3  asubuhi wakati mwalimu waliyekuwa wakimdai akiwa shuleni hapo akiendelea na majukumu yake.

Amesema mwalimu aliyedaiwa baada ya kuwaona wajasiriamali hao wakifika shuleni hapo na gari lao, ghafla alitimua mbio na kukimbilia kwenye shamba la mahindi karibu na shule hiyo ndipo mmoja kati yao alianza kumkimbiza. 

“Baada ya kushindwa kumkamata, alirejea katika eneo la shule na kuungana na mwenzake aliyekuwa amebaki kwenye gari na kwenda moja kwa moja walimvamia mwalimu mkuu aliyekuwa akizungumza na wazazi wa wanafunzi waliokuwa wamefika kulipa michango kisha kumkaba, kumkatia vishikizo vya shati na kupasua simu janja yake.

Wakati wajasiliamali hao wakifanya vitendo hivyo, wazazi waliokuwapo eneo hilo waliwakamata na kuwazuia wajasiliamali hao ndipo mwalimu mkuu alipokimbilia ofisini kwake na kujifungia ili kujinusuru na hasira za watu hao. 

''Wazazi hao walipowaachia wafanyabishara hao, walichukua mawe na kuanza kuponda mlango wa ofisi ambayo mwalimu mkuu alijificha na pia kukatakata matawi ya miti iliyoko shuleni hapo kwa hasira huku wakiwa kama wamepandisha kichaa kwa madai kuwa wanataka kulipwa fedha zao,'' amesema mwenyekiti wa kijiji.

Amelisema wanafunzi waliokuwa madarasani walikuwa wakishuhudia vurugu zinazotokea na baadhi yao walikimbilia kijijini kwenda kuwaita wazazi wao ili wakamsaidia mwalimu mkuu kwa kuwa waliona anapigwa na wafanyabishara hao waliovamia shule yao.

Kundi la wazazi limefika shuleni hapo baadhi wakiwa na silaha za jadi ndipo  wajasiliamali hao walipopanda gari lao na kuondoka katika eneo la shule na kutimkia kusikojulikana.

Mwenyekiti Pastory amesema mwalimu aliyekuwa anadaiwa alikopa redio, televisheni na vyombo mbalimbali vya ndani na alikuwa akisumbua kulipa na wakati mwingine alikuwa akiwakimbia wafanyabiashara hao kitendo kilichowapa hasira na kuamua kufanya vurugu shuleni hapo.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) Manispaa ya Sumbawanga, Mwalimu Huruma Kilingo, amewashauri walimu kuacha tabia za kukopa wakati wanajua hawana uwezo wa kulipa kwa kuwa vitendo kama hivyo vinaharibu haiba yao.

Pia amesema kwa mujibu wa sheria za utumishi ni makosa kufanya biashara katika maeneo ya shule na kitendo kilichofanyika kinapaswa sheria zichukuliwe ili kukomesha biashara katika maeneo hayo kwa kuwa wanawakosesha wanafunzi haki ya kupata masomo.