Migogoro mingi ya mali za urithi inasababishwa na kukosekana wosia- Makondo

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 03:10 PM Jul 10 2024
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mary Makondo, akitoa huduma ya msaada wa kisheria kwa mwananchi aliyetembelea banda la Mama Samia Legal Aid Campain kwenye maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar ed Salaam (DITF).
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mary Makondo, akitoa huduma ya msaada wa kisheria kwa mwananchi aliyetembelea banda la Mama Samia Legal Aid Campain kwenye maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar ed Salaam (DITF).

KATIBU Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo amesema migogoro mingi inayotokea wakati wa kugombania mali za urithi inasababishwa na kukosekana wosia kwa anayeacha mali husika.

Makondo alisema hayo wakati akizungumza na Nipashe kwenye banda la msaada wa Kisheria la Mama Samia maarufu Mama Samia Legal Aid Campaign kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea barabara ya Kilwa Temeke.

Alisema katika kampeni hiyo ya msaada wa kisheria ya Mama Samia, miongoni mwa kesi nyingi ambazo zimejitokeza katika mikoa saba ambayo kampeni hiyo imepita ni pamoja na hizo za mirathi.

"Kwenye masuala ya mirathi pia ni eneo ambalo limekuwa na mwitikio mkubwa kwa sababu migogoro mingi imekuwa ikitokea kwa sababu watu hawaandiki wosia,"alisema Makondo.

“Kwa hiyo kupitia kampeni hii ya Mama Samia Legal Aid Campaign, tutawasaidia wananchi namna gani wosia unapaswa kuandikwa, pale wapendwa wetu wanapokuwa wameondoka duniani na wameacha maandishi ya kuonyesha kwamba ni nani atakuwa mrithi.

"Ni nani atasimamia mali, na kufanya hivyo kunarahisisha taratibu za mahakama katika kuamua na hata kama yule ambaye ni msimamizi hafanyi vizuri, bado wanaweza kurudi mahakamani na kuomba kufutwa na kuwekwa mwingine."

Aliwataka wananchi kujenga tabia ya kuandika wosia ili kuepusha migogoro isitokee baadae pale wanapoondoka duniani.

“Kwa hiyo bado tunawasihi na kuwasisitiza wananchi tuandike wosia ili vile ambavyo tumevitafuta na kuvifanyia kazi, kuvipata kwa nguvu zetu, pale ambapo muda wa kuondoka duniani umefika, wale ambao wameachwa, watoto, wazee, wenzi, wasipate shida. Lakini tutakapoacha kuandika wosia, tutaamliwa na migogoro inakuwa mingi ya mivutano,"alisema Makondo.

“Kabla ya kuja hapa, nimepitia pia banda la mahakama, nimeongea na Kitengo Jumuishi cha Mahakama cha Temeke, wameniambia kwamba wanapokea kesi za mirathi zaidi ya 600 kwa wiki ambayo ni mingi sana.

"Lakini mingi ile ambayo kuna wosia inapopelekwa mahakamani inaenda haraka sana, ile ambayo haina inachukua muda mrefu kwa sababu wakati mwingine msimamizi anaweza akapotea inabidi atafutwe, warithi wanapata shida, wanachelewa, wengine ni wanafunzi wanasoma, kwa hiyo sisi tunawasihi muandike wosia kuhakikisha kwamba haki zinalindwa."

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi, miongoni mwa migogoro ambayo wametatua kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid Campaign katika mikoa saba waliyopita ni pamoja na ardhi, mirathi, ndoa na ukatili.