Meya za zamani Ubungo aibua mapya Simu 2000

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:09 AM Jul 10 2024
news
Picha: Mtandao
ALIYEKUWA Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob.

ALIYEKUWA Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, ameibuka na kutetea wafanyabiashara wa Soko la Simu 2000 wilayani humo baada ya kuibuka madai kuwa eneo hilo umepewa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ili ujenge karakana.

Amesema kama manispaa hiyo imechukua uamuzi wa kugawa eneo hilo kwa DART, atarudisha wafanyabiashara hao eneo la Ubungo Mataa walikokuwa wanafanya shughuli zao kabla ya kuhamia eneo hilo.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, Boniface aliandika jana kuwa Manispaa ya Kinondoni ilinunua eneo hilo lililokuwa na ekari tano kutoka kwa Shirika la Posta Tanzania wakati akiwa diwani mwaka (2010-2015) kwa madhumuni ya kuweka miradi ya uwekezaji ili kukuza mapato ya halmashauri.

Jacob alidai kuwa baada ya kununua eneo hilo, ikaligawa kwa matumizi ya stendi ya daladala, choo cha umma na soko la mazao na biashaara ndogo mwaka 2013 na kugawa vizimba vya soko kwa watu wasiostahili.

Alisema jambo hilo lilisababisha soko hilo kutokuwa na shughuli yoyote ya maendeleo kwa miaka miwili kwa kuwa waliopewa vizimba sokoni hapo siyo wafanyabiashara.

Alisema mwaka 2016, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, walianza utaratibu wa kuondoa machinga hao Ubungo Mataa na kuwapeleka maeneo rasmi bila mafanikio.

"Walipigwa mabomu, wakaharibu mali, wakafunguliwa kesi lakini machinga Ubungo Mataa hawakuondoka barabarani," alisema.

Alisema Mei Mosi, 2016, akiwa mstahiki meya na diwani wa manispaa hiyo, alifika eneo la Ubungo Mataa bila polisi na askari wa Jeshi la Akiba (Mgambo) na kuongea na wafanyabiashara hao na kuwaomba awapeleke eneo la Simu 2000.

"Niliwaambia kwa kuwa madiwani na watu wengine walipewa vizimba sokoni na maeneo nje ya soko wameshindwa kufanya soko lichangamke, basi kila mfanyabiashara wa Ubungo aende aingie pale sokoni Simu 2000, atakapochagua kukaa ndiyo pa kwake.

"Baada ya hotuba hiyo nilikwenda kwa maandamano mimi na wafanyabiashara wa Ubungo Mataa, tukaingia sokoni Simu 2000 kila mtu akakimbilia sehemu aliyoona inafaa," alisimulia.

Jacob alisema watu waliopita Ubungo Mataa siku hiyo walishangaa kukuta kukiwa safi na machinga wote walikubali kwenda soko la Simu 2000.

Alisema baada ya kugawanywa halmashauri, Ubungo iliwaomba wa Kinondoni wawachie Stendi ya Mawasiliano na soko hilo, na wao wakawaachia stendi na soko la Makumbusho na mali zingine waligawana kwa hisa za asilimia 60 Kinondoni na 40 Ubungo.

Alisema anashangazwa na uamuzi wa Baraza la Madiwani Ubungo la Julai 2024 kuamua kugawa eneo hilo muhimu na la kimkakati kwa mapato ya halmashauri na kutaka iwe karakana ya mabasi ya mwendokasi.

Alisema uamuzi uliochukuliwa bila kuwashirikisha wafanyabiashara hao utaliua soko hilo na kupoteza mapato ya halmashauri.

"Wanavunja soko wakati huu kukiwa na miundombinu ya zaidi ya Sh. billioni moja ambayo iliboresha mazingira ya soko la Simu 2000 kama ujenzi wa fensi, ujenzi wa mabanda ya soko, ujenzi wa choo sokoni, ujenzi wa vizimba, umeme na maji," alisema.

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wa Baraza la Madiwani , Meya wa Ubungo, Affary Juma Nyaigesha, alithibitisha baraza hilo limepitisha uamuzi wa kukabidhi DART eneo hilo, lakini haina maana ya kuwa wafanyabiashara hao wataondolewa.

Alisema katika awamu hii ya utawala uliojaa uhuru na haki serikali haiwezi kuondoa wajasiriamali ambao wanategemea eneo hilo kujipatia kipato.

Juzi asubuhi machinga wa eneo hilo waligoma na kuziba barabara kuzuia magari kuingia katika kituo cha mabasi, wakilalamikia uamuzi wa manispaa hiyo kuipa DART eneo hilo ili kujenga karakana ya mabasi ya mwendokasi.

Wakati wakiendelea na mgomo huo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Bomboko, kwa ajili ya kuzungumza nao walikataa na kumtaka aondoke kwa madai kuwa hawana imani naye.

Baadaye alifika Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila na kuwataka wafungue biashara zao kwa kuwa atakwenda kufanya kikao na DART, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na Manispaa ya Ubungo kisha atawaletea mrejesho Julai 13, mwaka huu.