Lissu ahofu fedha kupenyezwa CHADEMA

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 07:38 AM Aug 27 2024
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Picha:Mtandao
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ameonesha hofu ya kupenyezwa fedha ndani ya chama hicho ndiyo maana alilazimika kukemea suala la rushwa sababu alihisi kuna fedha zinaingizwa kutoka serikalini.

Kutokana na hofu hiyo, amesema kuna uwezakano jambo hilo likakivunja nguvu chama kutetea haki za Watanzania.

Lissu aliyasema hayo jana katika mahojiano na kipindi cha Dakika 45 kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ITV huku akisisitiza kuwa alilazimika kukemea jambo hilo ili kuonesha ukubwa na madhara ya tatizo hilo ndani ya chama.

Alisema alishtuka kuona katika kipindi cha uchaguzi, chama hicho kinakuwa na fedha ambazo hazijawahi kuwapo wala kutumika katika shughuli za kawaida za chama na kuhisi kuwa pengine zinatoka serikalini kama rushwa.

Pia, suala lingine lililompa shaka ni kufuatwa na watu na kumtaka abadilishe msimamo wake juu ya mambo anayoyakosoa anapokuwa kwenye hadhara, jambo ambalo halijawahi kutokea kwake tangu aingie kwenye siasa.

Kwa mujibu wa Lissu, suala hilo lilimpa shaka na kujiuliza maswali mengi na kumpa wasiwasi kuwa kama chama kinaruhusu rushwa, kuna uwezekano wa kukivunja nguvu ya utendaji kazi hasa katika kipindi ambacho nchi ina changamoto nyingi zinazohitaji kutatuliwa.

“Kama wanaweza kunifuata mimi nyumbani wakakaa na kuniambia hivi, nitakuwa niko peke yangu kweli? Nilijiuliza maswali mengi kwa hiyo sikwenda kuropoka kwenye mkutano wa hadhara. Kuna tatizo na linahitaji lisemwe hadharani ili lisikichafue chama chetu,” alisema.

Alisema maneno yanayoendelea kuwa kuna migongano ndani ya chama hicho  ni ya kawaida hasa katika kipindi hiki ambacho wanafanya uchaguzi wa ndani ule wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba, mwaka huu, na uchaguzi mkuu Oktoba 2025. 

“Katika uchaguzi wowote wanachama wanatafuta nafasi wawe viongozi wa chama. Wengine wanatafuta nafasi wawe wagombea wa chama na wawakilishi  katika uchaguzi wa serikali za mitaa, udiwani, ubunge na urais. Kwa hiyo, katika mwaka wa uchaguzi wa aina hii kusipokuwa na kelele hizo sio chama cha siasa,” alisema.

 Kwa miaka 20, alisema  amekuwa na uhusiano mzuri na Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, na hawajawahi kugombana wala kuvunjiana heshima.

Alisema tofauti za misimamo ya kisiasa kati yao zipo na ni jambo la kawaida  kwa sababu wao ni watu wenye mitizamo tofauti lakini kuna watu wanataka suala hilo lionekane kuwa ni ugomvi.

“Kwa mfano tunatofautiana kwenye suala la maridhiano. Mimi nadhani kwamba hili suala halitofika popote ni uongo tu, ni namna tu ya kupunguza joto na kukonga nyoyo za jumuiya za kimataifa ili serikali ipate jina zuri na misaada wakati mwenyekiti (Mbowe) alisema kupitia maridhiano tutafika,” alisema.

Kwa mujibu wa Lissu, kama wapinzani wanadhani chama hicho hakitaki maridhiano, wanakosea kwa sababu katika serikali ya  awamu ya tano chini ya Hayati John Magufuli, chama hicho kilitangaza hadharani kutaka maridhiano na serikali ili wazungumzie wimbi la watu kutekwa lililokuwa linaendelea.

“Tulipaza sauti ya maridhiano na Rais (Magufuli) alipogundua kwamba kufungulia watu kesi za uongo za ugaidi hakumlipi, akasema sasa tuzungumze. Tulipeleka mapendekezo yetu, juu ya mambo yanayohitajika kufanywa ili nchi iwe na maridhiano ya kweli, wameyakataa yote,” alisema.

Kuhusu kauli aliyoitoa hivi karibuni kuwa chama hicho si baba yake, alisema alikuwa na maana kuwa alihamia katika chama hicho kwa sababu alivutiwa na sera na itikadi na  ikitokea mambo hayo yakabadilika, anaweza kuondoka.

“CHADEMA ni chama cha siasa na tunaunganishwa na  itikadi fulani chenye mipango, sera, misimamo fulani, ikiondoka hiyo tutakutana kwenye urafiki wa mambo mengine lakini si masuala ya siasa,” alisema.

KUANZISHA CHAMA 

Kuhusu uvumi kwamba ana mpango wa kuanzisha chama, alisema hana mpango huo  kwa sababu mbalimbali ikiwamo mtazamo wake juu ya sera ya vyama vya siasa na ofisi ya msajili wa vyama kuwa vimewekwa kudhibiti upinzani.

“Mimi nianzishe chama halafu Jaji (Francis) Mutungi (Msajili wa Vyama vya Siasa) akisajili? Eeh  itabidi tusubiri karne nyingine. Sijafikiria kuanzisha chama kingine wala kuhama CHADEMA na sababu ndizo hizo,” alisema.

Alisema licha viongozi wa chama hicho akiwamo yeye kuongoza kushtakiwa kwa uchochezi hajawahi kukutwa na hatia hata mara moja na hakuna kesi iliyofika mwisho.  

SERA MPYA YAJA

Kwa sasa, Lissu alisema chama hicho kiko kwenye mchakato wa kutengeneza sera ya jinsia na makundi maalum ikiwa ni maelekezo kutoka katika Sheria ya Vyama vya Siasa iliyofanyiwa maboresho hivi karibuni.

Alisema kuna haja ya kuangalia upya sheria ya vyama vya siasa kipengele cha vigezo vya chama kupata ruzuku ili chama kipewe ruzuku kulingana na asilimia ya wabunge wa majimbo, madiwani iliyopata.

“Kama fungu lote ndio asilimia 100 ya kura kwa nini chama kinachopata asilimia moja kisipate ruzuku, kwa nini inaanzia asilimia tano tu? Mimi nahisi kuna ufisadi unaendelea hapo,” alisema.

Alisema kwa sheria ilivyo sasa chama kitapata  ruzuku  kama katika uchaguzi uliopita kilipata wabunge wa majimbo, madiwani wa kata au asilimia tano  au zaidi ya kura zote halali zilizopigwa kwa wabunge jambo analodhani kuwa si sawa kwa vyama vingine vya siasa.

KUIBURUZA TUME KORTINI 

Alisema chama hicho kimepanga kwenda mahakamani ili kujua msimamo wa Tume ya Uchaguzi juu ya ushiriki wa Ofisi ya Rais -Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika uchaguzi wa serikali za mitaa  kwa kuwa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi iliyotungwa hivi karibuni imewanyang’anya mamlaka hiyo.

Alisema katika marekebisho ya sheria za uchaguzi  mwaka huu kulitungwa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi  yenye kipengele kinachoeleza kuwa tume hiyo ndio yenye mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa vijiji na wa mitaa kwa kufuata utaratibu utakaowekwa kwenye sheria itakayotungwa na bunge.

Alisema kwa maana hiyo TAMISEMI  na waziri wake, Mohamed Mchengerwa, hawana mamlaka ya kusimamia uchaguzi huo, hivyo wanashangazwa kuona kuwa waziri huo anatoa tangazo la uchaguzi.

Alisema pia ametia nia kugombea nafasi ya rais wa Tanzania kwenye chama chake hivyo kama vikao vya chama vikimpitisha atawania kiti hicho.