RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameelezea mafanikio ya serikali yake katika kipindi cha mwaka 2024 ikiwamo kukuza uchumi kwa kuongeza udhibiti na ukusanyaji wa mapato.
Rais Mwinyi ameweka hayo bayana katika risala yake za kuuaga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka 2025.
Alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuimarisha uwekezaji na biashara, ujenzi wa miundombinu ya barabara mijini na vijijini, viwanja vya ndege na bandari, ujenzi wa nyumba za makaazi, usambazaji wa huduma za umeme na majisafi na salama pamoja na uimarishaji wa sekta ya elimu na afya kote nchini.
Kadhalika, alisema serikali yake imefanikiwa kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuanzisha programu za utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa makundi ya wananchi na kuwajengea mazingira bora ya kufanya biashara hasa baada ya kufunguliwa rasmi kwa masoko makubwa ya kisasa ya Mwanakwerekwe na Jumbi.
Pia, ameeleza mafanikio aliyoyapata kupitia sekta ya michezo na kwamba tayari serikali yake inakamilisha mwaka 2024 ikiwa imepiga hatua kubwa katika kuimarisha sekta ya michezo kwa mafanikio baada ya kufanya ukarabati mkubwa wa viwanja vya michezo vya Amani Complex, Gombani, sambamba na ujenzi wa viwanja vya michezo mbalimbali pamoja na hoteli ya Amani.
“Jitihada hizi zinalenga kuzidi kuimarisha sekta ya michezo na kuchochea shughuli za utalii kupitia michezo na matamasha. Aidha, tumedhamiria kuwa na miundombinu ya michezo yenye kukidhi mahitaji ya mashindano ya CHAN mwaka 2025 na ya Afcon mwaka 2027 yatakayoandaliwa kwa pamoja kati ya Tanzania, Kenya na Uganda,” alisema Rais Mwinyi.
“Tuna wajibu mkubwa wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa katika nchi yetu na kutokana na misingi hiyo, nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika jitihada zetu za kukuza uchumi, kuimarisha miundombinu, biashara na uwekezaji, huduma za jamii na kuimarisha demokrasia na utawala bora.”
Rais Mwinyi alisema mafanikio mengine yaliyopatikana katika mwaka 2024, yataelezwa na mawaziri wake.
RAI KWA WAFANYAKAZI
Alitoa rai kwa wafanyakazi wote kuongeza kasi ya kufanya kazi kwa bidii zaidi kwa mwaka ujao kila mtu kwa nafasi yake katika kufanikisha jitihada za kujiletea maendeleo.
UCHAGUZI MKUU
Rais Mwinyi alisema tayari serikali zote mbili; Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Tume za Uchaguzi, NEC na ZEC zimeanza kuchukua hatua za matayarisho kuhakikisha nchi inaendesha uchaguzi kwa misingi ya haki na sheria.
Alitaka wananchi kuendelea kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
“Ni wajibu wa viongozi wa kisiasa, taasisi za kijamii, viongozi wa dini, na wanachi wote kukumbushana umuhimu wa kudumisha na kuilinda amani tuliyonayo ili tuzidi kupiga hatua za maendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na wale watakao kuja baada yetu.
“Tunapoukamilisha mwaka huu wa 2024, navishukuru sana na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na amani kwa wananchi pamoja na wageni wanaoitembelea nchi yetu,” alisema Rais Mwinyi.
AHADI 2025
Rais Mwinyi alisema serikali yake itaendelea kuhakikisha amani iliyopo inaendelea kudumu na kuahidi kuongeza kasi ya utekelezaji maendeleo.
“Niwaombe wananchi waendelee kuipa serikali ushirikiano hasa kwa kudumisha amani, umoja na mshikamano ili kwa pamoja kupiga hatua za maendeleo tunayoyatarajia. Nachukua fursa hii kutoa salamu za mwaka mpya kwa wananchi wote wa Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, natoa salamu kwa viongozi wa serikali na nchi rafiki, taasisi za kimataifa na washirika wetu wote wa maendeleo.”
SHEREHE YA MIAKA 61 YA MAPINDUZI
Akizungumzia sherehe za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Mwinyi alisema tayari shughuli mbalimbali za maadhimisho ya sherehe hizo zimeshaanza tangu 15 Desemba kwa usafi wa mazingira katika maeneo mengi ya nchi.
Alitoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika matukio mbalimbali yaliyoandaliwa kwa ajili ya sherehe hizo ikiwa ni hatua ya kuonesha uzalendo na kuthamini jitihada za waasisi za kufanya Mapinduzi ili kuikomboa nchi.
“Matukio hayo yanajumuisha uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi, shughuli za michezo na utamaduni na yatafikia kilele chake Januari 12 katika uwanja wa Gombani Pemba,” alisema Rais Mwinyi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED