KESI KUCHOMA MKE KWA MKAA: Sajenti: Mshtakiwa aliamua kusema ukweli awe huru

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:37 AM Nov 07 2024
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imepokea maelezo ya onyo ya mshtakiwa 
Khamis Luwonga (38), anayetuhumiwa kumuua mkewe Naomi Marijani na kisha kumchoma moto mwili kwa kutumia magunia mawili ya mkaa kama kielelezo namba moja katika kesi hiyo.
Picha: Grace Gurisha
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imepokea maelezo ya onyo ya mshtakiwa Khamis Luwonga (38), anayetuhumiwa kumuua mkewe Naomi Marijani na kisha kumchoma moto mwili kwa kutumia magunia mawili ya mkaa kama kielelezo namba moja katika kesi hiyo.

SAJENTI William Christopher (51) amedai mahakamani kuwa mshtakiwa Khamis Luwongo (38) anayedaiwa kumuua mkewe Naomi Marijani na kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa, aliamua kusema ukweli kwa madai kuwa anataka kuwa huru.

Pia amedai alikatisha kumchukua maelezo ya onyo yaliyoanza kuanzia saa tano asubuhi hadi saa saba mchana, baada ya kueleza jinsi alivyomuua mke wake na kumchoma moto nyumbani, hivyo ikawabidi wahamie eneo la tukio.

Sajenti Christopher alidai hayo jana mbele ya Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati akitoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa huku akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Yasinta Peter.

Alidai kuwa Julai 16, 2019, akiwa ofisini kwake Kanda Maalumu Dar es Salaam - Kitengo cha Uhalifu wa Mtandao, aliitwa na bosi wake ASP Ahmed Makelle ili awakutanishe na mshtakiwa kumhoji kuhusiana na mawasiliano baina yake na mkewe.

"Nilipewa utambulisho na ASP Makelle kuwa 'huyu ndiye mume wa Naomi aliyepotea, kuanzia hapo nikamjua, nikampeleka ofisini kwangu, nilikuwa mimi na yeye tu.

"Nikaanza kumwuliza maswali, akaniambia anatumia namba ya simu 0714 812530 na ya mke wake ni 0655 527203 na mke wake alipotea tangu Mei 15, 2019, asubuhi hadi siku hiyo (Julai 16, 2019," alidai Sajenti Christopher.

Alidai kuwa alimwuliza mshtakiwa kama mkewe Naomi aliondoka na simu zake na laini? Na pia alimwuliza kama walishawahi kuwasiliana kwa kipindi chote hicho, akasema walikuwa wakitumiana ujumbe mfupi.

"Nikamwuliza 'mbona zipo kwenye handset' moja unazozitumia wewe? Akashindwa kunipa jibu na alishindwa kunijibu kama walishakutana tena, ndiyo akatoweka kwa mara ya pili," alidai Sajenti Christopher.

Baada ya kushindwa kujibu maswali hayo, alimweleza Sajenti  Christopher, akimnukuu kwamba alisema "ngoja tu nikueleze ukweli kwa sababu hata nikinyamaza siwezi kuwa huru". Akadai alimuua mkewe Naomi.

Kwa kauli hiyo ya mshtakiwa Luwongo, maarufu Meshack, ilitoa mabadiliko ambayo ilimbidi Sajenti Christopher atoke hapo, mshtakiwa akahojiwe kwa kuandikwa maelezo ya onyo kwa kuwa amekiri kufanya uhalifu wa kumuua mke wake.

"Nilianza kumhoji kuanzia saa tano asubuhi ya Julai 16, 2019, ambapo tulisitisha mahojiano saa saba mchana baada ya kueleza tukio alilifanya nyumbani kwake Gezaulole.

"Nilirudi kwa bosi wangu ASP Makelle kumweleza kuwa mshtakiwa amekiri kosa, wanajiandaa kwenda nyumbani kwake, walipofika alionesha eneo lote la tukio hadi sehemu alipomchomea na alipofukia mabaki na majivu ya mwili wa marehemu," alidai.

Alidai kuwa baada ya kumaliza tukio hilo, walirudi kituo cha polisi saa 5:45 usiku, aliandika maelezo ya nyongeza, walimaliza saa 6:20 usiku.

Jaji Mwanga alipokea maelezo hayo ya onyo ya mshtakiwa kama kielelezo namba moja katika kesi hiyo.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba nne ya mwaka 2019, mshtakiwa Luwonga ambaye ni Mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa Mei 15, 2019, akiwa Gezaulole, Kigamboni, Dar es Salaam, alimuua Naomi Marijani.