JANGA UKIMWI... Tabia bado ni donda sugu

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 04:58 AM May 24 2024
Kipimo cha HIV.
Picha: Mtandaoni
Kipimo cha HIV.

WADAU wa sekta ya afya wameshauri serikali kuweka mazingira rafiki kwa vijana katika vituo vya afya kukabiliana na janga la maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU).

Ni baada ya ripoti mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa juzi kuonesha bado kuna kiwango kikubwa cha watu wanaoambukizwa VVU, homa ya ini na magonjwa ya zinaa.

Wakitoa maoni yao kuhusu ripoti hiyo inayoonesha zaidi ya watu milioni moja wa umri wa kuanzia miaka 15 hadi 49 wanaambukizwa kaswende na kisonono kila mwaka, wadau hao walisema jana kuwa wanataka kundi hilo liwekewe mazingira rafiki kwa kuwa ndilo lenye shida.

Akizungumza na Nipashe jana juu ya ripoti hiyo ya WHO, mdau wa masuala ya afya kwa vijana, Catherine Madebe, alisema kwa upande wa Tanzania, changamoto wanayokutana nayo ni rika la vijana wa umri wa kuanzia miaka 15 hadi 24, hawaendi hospitalini kupima kama wana maambukizi.

Alisema wanapoona dalili hukimbilia katika maduka ya dawa kununua dawa na si kupima kujua wana maambukizi ya aina gani.

Catherine alitaja changamoto nyingine ni vijana kutumia kwa kiwango kikubwa dawa za antibaiotiki ambapo hadi afike hospitalini anakuwa tayari na usugu wa dawa.

Alisema hali ya uelewa sahihi wa matumizi ya kondomu kwao ni asilimia 40 licha ya kujua umuhimu wake. Kuna changamoto kwenye kutumia kinga hizo dhidi ya maambukizi ya VVU.

Kutokana na changamoto hizo, Catherine alisema ushirikishwaji wa pamoja kati ya wadau na serikali ni jambo muhimu, hivyo uongezwe.

Alisema serikali inapaswa kutoa elimu juu ya VVU/UKIMWI kwa kuzingatia rika tofauti, hasa kwa vijana, ili wanapoona taarifa husika wapate ujumbe moja kwa moja.

Alisema kuwa mazingira ya hospitalini si rafiki kwa vijana kuzungumza masuala ya afya kuanzia kujikinga.

Mdau huyo alisema wamepiga kelele juu ya suala hilo na sasa kuna baadhi ya vituo vimeweka huduma hizo ingawa si vingi, na kutaka kasi iongezwe ili vijana wapate mahali sahihi pa kwenda.

"Tufanye hivyo ili tuwaambie vijana kuwa sasa hivi tumeshawawekea mazingira rafiki, hivyo ukiwa na changamoto ya kiafya usikimbilie katika duka la dawa na kuchukua dawa na kutengeneza usugu, waende moja kwa moja hospitalini au katika vituo vya afya," alisema.