GCLA yatadharisha wananchi kutumia jiwe kuondoa sumu ya nyoka

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 11:02 AM Jul 10 2024
Wananchi wakiendelea kupata elimu katika Banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) katika Maonesho ya 48  ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, mkoani Dar es Salaam
PICHA:MPIGAPICHA WETU
Wananchi wakiendelea kupata elimu katika Banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, mkoani Dar es Salaam

MAABARA ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imewatahadharisha wananchi wanaopata ajali ya kung’atwa na nyoka kutotumia mawe kuondoa sumu na badala yake kuwahi kituo cha afya kupata matibabu haraka.

Tahadhari hiyo ilitolewa na Mratibu na Msimamizi wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu GCLA, Yohana Goshashy, wakati akuzungumza na waandishi wa habari kwenye banda la GCLA katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Watu wengi wanaokuja hapa wanauliza kuhusu kutumia jiwe kuondoa sumu kwa mtu aliyeng’atwa na nyoka, wataalam tunaonya kwasababu siyo kila mtu anafahamu kuhusu aina ya sumu za nyoka na hivyo inaweza kuleta madhara makubwa kwa aliyeng’atwa,” alisema.

Alisema kuna aina nyingi za sumu ambazo wananchi hawazifahamu nyingine zinawahi kusambaa mwilini kwa haraka na kusababisha kifo.

Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kujifunza na kufuatilia taarifa za matukio ya sumu kupitia vyombo vya habari ili kuondokana na matatizo yanayotokana na kukosa uelewa.

Goshashy alisema wananchi wengi waliuliza pia kuhusu madhara ya sumu zitokanazo na pombe na kudhani mamlaka hazifanyi kazi za kuelimisha na kuzuia matumizi kupita kiasi.

Alisema mamlaka zinatekeleza wajibu wao wa kuelimisha ila hazina mamlaka ya kuingilia uhuru wa watu kutumia vinywaji hivvyo kupita kiasi.

“Ndio sababu tunaendelea kutoa elimu ili watu wafahamu na kuondokana na changamoto hizi za unywaji wa pombe kupita kiasi na tunawaleza madhara yake ikiwamo kuharibu Figo na hata kusababisha kifo,” alisema Goshashy.

Aliwataka wananchi kuendelea kujitokeza kwenye banda hilo kufahamu huduma wanazotoa na kusikiliza maoni yao ili wapate uelewa wa kutosha.

Alishauri watu wanaopata matukio ya sumu watoe taarifa katika kituo cha afya kilicho karibu au kupiga simu kituo cha matukio ya sumu kwa namba 0736623333.