Dk. Mpango ataka msukumo utolewe kwa vijiji na vitongoji visivyo na umeme

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:24 AM Jul 10 2024
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.
Picha: Mpigapicha Wetu
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango ambaye yupo katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Kigoma, ameiagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa inatoa msukumo wa upatikanaji umeme kwa vijiji na vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na huduma hiyo.

Dk. Mpango ameyasema hayo jana Julai 9, 2024, wakati akikagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali mkoani Kigoma ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake mkoani humo.

Akiwa katika Kata ya Kalinzi na Mnanila Jimbo la Buhigwe, Dk. Mpango alisema kuwa, changamoto za umeme kwa sasa zinashughulikiwa vizuri ambapo  ameipongeza Wizara ya Nishati na watendaji kwa ujumla kwa kazi nzuri wanayofanya kwenye utekelezaji na usimamizi wa miradi ya Sekta ya Nishati.

Akijibu hoja mbalimbali wakati wa ziara hiyo, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, aliwaagiza TANESCO na REA kuhakikisha vijiji 5 vilivyokosa umeme kwenye Kata ya Kalinzi vinapatiwa umeme kwa kuanza na vijiji 3 ambavyo wakandarasi wako kwenye eneo la mradi huku vifaa vikiwa tayari vimeshapelekwa.

1

Alivitaja vijiji hivyo vitatu kuwa ni Bugamba, Kigadye, na Kiziba ambapo alieleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ilichelewa kwa sababu ya mvua kubwa na Ziwa Tanganyika  kujaa ila kwa sasa utekelezaji wake unakwenda kutekelezwa.

‘’ Niwahakikishie wananchi wa Kalinzi na maeneo yote yenye changamoto ya umeme tunakwenda kuwafikia na miradi inakwenda kuanza ikiwemo miradi ya vitongoji, ujazilizi na  vijiji miji."’ alisema Kapinga.

Aliongeza kuwa, vitongoji 15 vya kata hiyo vinakwenda kupatiwa umeme na kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 vitongoji 4,000 vimetengewa fedha nchini ambapo wananchi wa Kalinzi pia ni wanufaika.
2

Kapinga alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Buhigwe kwa ufuatiliaji mzuri wa miradi na kuahidi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati iko imara kuhakikisha wananchi wanapata umeme.

Akiwa kata ya Mnanila,  Kapinga aliwahakikishia wananchi kuwa vitongoji 107 vya jimbo la Buhigwe na Kata ya Mnanilwa ambavyo bado havijapatiwa umeme vitapatiwa na tayari wakandarasi wameanza utekelezaji wa miradi hiyo  chini ya wakala wa Nishati Vijijini (REA).
3

Makamu wa Rais katika ziara hiyo  aliongozana na Mawaziri mbalimbali na Naibu Mawaziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, TAMISEMi, Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maji, Wabunge kutoka Mkoa wa Kigoma pamoja na viongozi wa Wizara ya Nishati wakiongozwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Innocent Luoga.