Dar sasa kupambwa na taa na kamera za usalama

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 04:41 PM Oct 23 2024
Chalamila aanza ziara ya usiku kwa usiku
Picha: Mpigapicha Wetu
Chalamila aanza ziara ya usiku kwa usiku

MKOA wa Dar es Salaam umeanza kuweka taa na kamera za usalama katika maeneo mengi ya jiji hilo kama mkakati wa kurahisisha usalama na kuwawezesha wafanyabiashara kufanyabiashara kwa saa 24.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila, wakati wa ziara yake usiku kwenye maeneo mbalimbali ya jiji hilo. 

Chalamila alitembelea kukagua ujenzi wa barabara ya mwendokasi (BRT III), inayoanzia maeneo ya Posta hadi Gongo la Mboto, shule ya Azania na Jangwani na soko la Kariakoo.

Akiwa kwenye shule ya sekondari Azamia na Jangwani, Chalamila aliagiza siku ya Jumamosi kuwe na Bonanza baina ya shule ya Azania na Jangwani hali iliyowafanya wanafunzi hao kulipuka kwa shangwe.

Chalamila alisema watahakikisha maeneo mengi yanakuwa na taa na kamera za usalama ili kila atakayefanya uhalifu afahamike na kuchukuliwa hatua za kisheria kama fundisho kwa wengine.

 “Hivi karibuni nilitembelea moja ya nchi zilizoendelea, mwanamke mmoja aliibiwa pochi yake lakini ndani ya saa saba aliitwa akaonyeshwa aliyemwibia na pochi yake ikapatikana sasa jiulize kwa sasa hapa Kariakoo mtu akiiba pochi itapatikana kirahisi namna hiyo,” alihoji 

“Ndiyo maana tunataka kuupendezesha mji wa Dar es Salaam kwa kuupamba na taa na kamera kiasi kwamba watu wanaotoka mikoani wakifika tu wajue kwamba hapa ndiyo Dar es Salaam. Kuna kampuni imejitolea kwamba inaweza kufunga taaa za mfano na mkiridhika nazo wapeni kazi hiyo,” alisema 

Alisema Manispaa za Jiji hilo zimeshaanza kufunga taa kwenye baadhi ya maeneo na aliagiza kazi hiyo iwe endelevu na ikamilike ndani ya muda mfupi ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanyakazi wakiwa na uhakika wa usalama na biashara zao. 

Akizungumzia soko la Kariakoo, Chalamila alisema soko hilo lilikarabatiwa kwa bilioni 28 na umefikia zaidi ya asilimia 92 na majina ya wafanyabiashara watakaokuwa kwenye soko hilo yanahakikiwa kwa awamu ya tatu.

1

 Alisema baada ya kuhakikiwa yataingizwa kwenye mfumo kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ili soko hilo liweze kufunguliwa na kuanza kufanya kazi haraka.

 Alilipongeza Shirika la Nyumba (NHC), kwa uamuzi wake wa kuyavunja majengo ya zamani na kuingia ubia na wafanyabiashara binafsi kwaajili ya kujenga majengo marefu ya kupangisha na biashara.

 Alisema ujenzi wa majengo hayo marefu utaipendeesha Kariakoo kuwa mji wa kisasa na unaovutia kwani majengo yaliyoko yamechakaa na hayachukui wapangaji wengi kama itakavyokuwa kwa majengo mapya yatakapokamilika.

 “Majengo mengi yatakuwa ya orofa zaidi ya 10 na  kutakuwa na maduka na makazi ya kupanga ambayo yatawarahishia wafanyabiashara kutoka mikoa mbalimbali na mataifa ya kigeni kupata makazi ya muda wanapokuja kuchukua mizigo,” alisema Chalamila.

 “Kwa sasa mabasi yanafanyakazi saa 24 kutoka mikoa mbalimbali swali limebaki je abiria watakaposhuka wataelekea wapi hasa wale ambao wanakuja kuchukua mizigo Kariakoo? ndiyo maaga Rais akaagiza kwa kuwa ruti za mabasi ni saa 24, safari za ndege na SGR upo ni vyema Kariakoo ikawa wazi kwa saa 24,” alisema

 Meya wa Jiji la Ilala, Omar Kumbilamoto, alisema mapendekezo yatakayoletwa kwenye baraza la madiwani kuhusu mipango ya kuboresha Jiji kwa kuweka kamera na taa za usalama yatapitishwa kwa utekelezaji wa haraka.

 “Nampongeza Mkurugenzi wa Jiji la Ilala kwa maono yake ya kuhakikisha linakuwa na taa na kamera za kutosha, tumepakana na Wilaya za Mkoa wa Pwani na Wilaya mbalimbali kwa hiyo nikuhakikishie tutaweka taa ili watu wote wakifika Dar tu waone mwanga wa kutosha hatutaki kuona maeneo yetu yako gizani,” alisema

 Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa bilioni 28 za ukarabati wa soko la Kariakoo lilipoungua na shilingi milioni 100 zilizotumika uwajengea wafanyabiashara waliokuwa hapo maeneo ya muda.

2