TCRA yataka umakini matumizi akili mnemba

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:22 AM Oct 23 2024
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari.
Picha:Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari.

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imezitaka taasisi mbalimbali kuwa makini zinapochakata taarifa kwa kutumia akili mnemba (Artificial Inteligence - AI) ili kuepuka upotoshaji.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari, aliyasema hayo jana katika mkutano uliojadili namna taasisi zinavyoweza kupata thamani kubwa wakati wa uchakataji wa taarifa walizonazo na kuboresha huduma zao.

Mkutano huo ulioandaliwa na Umoja wa Wakuu wa Kampuni na Taasisi (CEO Roundtable) uliwakutanisha pamoja wakuu wa taasisi binafsi na za serikali jijini Dar es Salaam.

Aliwakumbusha kuwa taarifa wanazoziweka kwenye Akili Mnemba ziwe zimekusanywa kwa misingi ya kisayansi ili ziwe sahihi, kinyume cha hapo wanaweza kutoa taarifa za kupotosha jamii kwa kuwa mfumo huo hauna uwezo wa kutambua kuwa taarifa hizo sio za kweli.

Dk. Jabir alisema licha ya AI kuwa na uwezo wa kuchakata taarifa na kufanya uamuzi kama binadamu, ili zifanye kazi ipasavyo ni lazima kuwe na taarifa nyingi zilizochakatwa ielekezwe ni aina gani ya taarifa inahitajika kutoka kwenye takwimu hizo.

Alisema AI inaweza kuchagiza ukuaji wa biashara kama ikitumiwa vizuri, akielekeza  kuwa taarifa inapaswa ichakatwe vizuri ndipo iingizwe katika mfumo huo kwa ajili ya kusaidia kutafasiri kwa aina tofauti.

“Kwa hiyo Akili Mnemba inakuja huku mwisho kabisa kwamba umeshachakata takwimu zako zile, ndio unaweza kuitumia,” alisema.

Alisema wameamua kuwa na vikao vya aina hiyo baada ya kugundua kuwa kuna taarifa nyingi zinakusanywa katika taasisi, hivyo ni muhimu kukutana pamoja kujadili namna wanavyoweza kuziongeza thamani na wazitumie kuboresha huduma zao.

“Wanaweza kupata aina ya bidhaa au huduma ambayo hapo awali walikuwa hawaipati au wakaboresha huduma zikawa bora zaidi kutokana na kuwa na uwezo wa kuzitafsiri takwimu au taarifa walizonazo,” alisema.

Aidha, alisema mkutano huo ni muhimu kwa sababu kampuni hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa sana katika ukuaji wa uchumi wa kidigiti hivyo taarifa wanazozikusanya zina mchango mkubwa katika kuboresha biashara zao.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Soft Tech, Harish Bhatt, alisema takwimu zinasaidia kampuni kufanya uamuzi wa namna ya kuboresha biashara na kutoa huduma nzuri kwa wateja.

Alitolea mfano katika benki wanaweza kutumia takwimu kuamua aina gani ya mteja kumpa mkopo wa aina gani ili kupunguza hasara.

Mkuu wa Huduma, Masoko na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Norman Kiondo, alisema kama kampuni inahusika na ukusanyaji wa takwimu wamejifunza namna taarifa inavyoweza kusaidia wafanyabiashara kuboresha kazi zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa CEO Roundtable, Santina Benson, alisema waliamua kuziweka katika meza moja taasisi binafsi na serikali, ili kujadili wazitumie vipi taarifa walizonazo ili kuboresha mazingira ya biashara zao.

Alisema wazo hilo lilizaliwa katika mkutano kama huo uliofanyika mwaka jana ambapo katika majadiliano yao waligundua kuwa wanataarifa nyingi, lakini hawafahamu namna ya kuzitumia ili kuboresha huduma zao.