Diarra atoa siri kumzuia Ateba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:48 AM Oct 23 2024
Diarra atoa siri  kumzuia Ateba
Picha:Mtandao
Diarra atoa siri kumzuia Ateba

GOLIKIPA namba moja wa Yanga, Djigui Diarra, amefunguka kwa mara ya kwanza baada ya mchezo wa dabi uliopigwa Jumamosi iliyopita, Uwanja wa Benjamin Mkapa na kueleza mbinu alizotumia kuokoa hatari kutoka kwa Leonel Ateba, ambayo ingeweza kuipatia Simba bao la kuongoza dakika ya nne tu ya mchezo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, kipa huyo raia wa Mali, alisema pamoja na kucheza michezo kadhaa ya dabi nchini, lakini mechi ya Jumamosi ambayo Yanga ilishinda bao 1-0, ilikuwa ni bora zaidi kuliko zote alizocheza.

"Mechi yangu bora ya Simba na Yanga tangu nifike hapa ni hii ya juzi ya ushindi wa bao 1-0, kwa sababu nilirejea nchini siku ile ile ya mechi, sikuwa fiti sana, nilikuwa na uchovu mkubwa, lakini viongozi wa Yanga, makocha, waliniweka sawa kisaikolojia na kuweza kukaa langoni, ukweli ni mechi bora mno kwangu," alisema kipa huyo.

Diarra alikuwa ametoka kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Mali ambacho kilicheza mchezo wake Oktoba 15, mwaka huu, kikiwa ugenini nchini Guinea Bissau ambapo alikaa langoni na timu hizo kutoka suluhu.

Kabla ya hapo alikaa langoni katika mchezo wa kwanza dhidi ya timu hiyo, Mali ikicheza nyumbani, Oktoba 11 na kushinda bao 1-0, katika mechi za Kundi I, kuwania kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), zinazotarajiwa kuchezwa mwakani nchini Morocco, kundi hilo likizishirikisha pia nchi za Msumbiji na Eswatini, zamani Swaziland.

Akisimulia jinsi alivyookoa hatari ambayo ilitokea pale straika Mcameroon, Ateba alipokuwa akijaribu kumpiga chenga, alisema siku nyingi alishamsoma mchezaji huyo jinsi anavyocheza, hivyo hakuokoa kwa bahati mbaya.

Alisema yeye ni golikipa, hivyo mbali na mazoezi ya uwanjani, hutenga pia muda wa kuwasoma wapinzani mbalimbali wanaoweza kukutana nao, hasa mastrika jinsi wanavyofunga mabao yao, ili hata ikitokea ajue namna ya kukabiliana nao.

"Huwa naangalia mechi za Simba, nawajua, kwa hiyo nilipoona tumebaki mawili na tayari nimeshamsoma anavyocheza, nilifahamu akipata mpira eneo lile atafanya nini.

"Nilijua ataenda kushoto, hivyo sikuwa na presha na kweli akafanya hivyo, nikaokoa, sikuhama eneo, nikasimama pale pale maana nilijua unaweza kumfuata mpinzani naye ataupiga muda ule ule, na kweli nikaokoa tena," alisema Diarra ambaye alijiunga na Yanga mwaka 2021, akitokea Klabu ya Stade Malien ya jijini Bamako nchini Mali.

Katika tukio hilo, Ateba alitaka  kumpiga chenga Diarra, lakini haikufanikiwa, badala yake kipa huyo raia wa Mali, alifanikiwa kuukoa kwa mkono wake wa kulia, aliporuka upande wake wa kulia, ambao ni wa kushoto kwa straika huyo.

Kama vile haitoshi mpira aliookoa Diarra ulikwenda kwenye mguu wa kulia wa Joshua Mutale, ambaye alitandika shuti lililombabatiza kipa huyo na kuiokoa Yanga kwenye shambulizi hatari zaidi katika mchezo  ambao Simba walilifanya.