Manula arejeshwa Stars kusaka tiketi ya CHAN

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:52 AM Oct 23 2024
GOLIKIPA wa Simba, Aishi Manula.
Picha:Mtandao
GOLIKIPA wa Simba, Aishi Manula.

GOLIKIPA wa Simba, Aishi Manula, ni mmoja wa wachezaji 24 walioteuliwa kuunda kikosi cha timu ya soka, Taifa Stars, kitakachoingia kambini kucheza mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), zitakazofanyika mwakani.

Taarifa iliyotolewa jana mchana na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), limesema Bakari Shime, ambaye atakuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho, ameteua kikosi hicho cha wachezaji wanaocheza ligi ya ndani kwa ajili ya mchezo wa mtoano dhidi ya Sudan unaotarajiwa kupigwa kati ya Oktoba 25 hadi 27, huku marudiano yakitarajiwa kuchezwa kati ya Novemba Mosi hadi 3, mwaka huu.

Fainali za CHAN zinatarajiwa kucheza nchini Tanzania, Kenya na Uganda kuanzia Februari Mosi hadi 28, mwakani.

Hata hivyo, uteuzi wa Manula umekuja wakati kipa huyo akiwa hana namba katika klabu yake ya Simba, na si kucheza, bali amekuwa hakai hata benchi.

Mbali na Manula, wachezaji wengine wanaocheza ligi ya ndani walioitwa kwenye kikosi hicho ni Isaya Kasanga kutoka TFF Academy TDS, akiichezea pia timu ya Prisons chini ya miaka 17.

Wengine ni Antony Mpenda kutoka Azam chini ya miaka 20, Nickson Mosha (KMC), Lameck Lawi (Coastal Union), Vedatus Masinde (TMA FC inayocheza Ligi ya Champioship), Hijjah Shamte (Kegar Sugar), Abdulkaris Kiswanya (Azam chini ya miaka 20), Shekhan Khamis (Yanga), Ahmed Pipino (Magnet FC), Sabri Kondo (KVZ), Bakari Msimu (Coastal Union) na Velentino Mashaka kutoka Simba.

Wachezaji wote waliotajwa hapo juu wanaichezea pia Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes.

Wachezaji wengine ambao hawapo Ngorongoro Heroes, mbali na Manula na Kasanga ni Paschal Msindo na Adolf Mtasingwa wote wa Azam FC, David Brayson na Ismail Kada wa JKT Tanzania, Ibrahim Ame na Cyprian Ngushi wa Mashujaa FC, Charles Semfuko wa Coastal Union, Salum Ramadhani kutoka KenGold, na kinara wa mabao Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na mabao sita, Selemani Mwalimu wa Fountain Gate.