JUMUIYA ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar imeadhimisha miaka minne ya mafanikio ya uongozi wa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwenye sekta ya afya, elimu, miundombinu ya barababra na utalii.
Akiongoza mjadala katika kongamano hilo lililohudhuriwa na wana-CCM pamoja na mawaziri wa SMZ lililofanyika visiwani hapa, Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk. Ayoub Rioba, alisema yapo mafanikio mengi yaliopatikana katika uongozi wake Dk. Mwinyi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu wa CCM, Dk. Stephen Wasira, akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM na umuhimu wa watu kujiandikisha kupiga kura, alisema miaka minne iliyopita, Dk. Hussein aliongoza bendera ya kuiongoza Zanzibar na mafanikio yaliyopatikana ni mengi ikiwamo kukua kwa uchumi na makusanyo ya mapato serikalini yameongezeka na kutia moyo.
Alisema ongezeko hilo limenufaisha jamii ya Zanzibar na kutoa mfano wa pensheni ya wazee imeongezeka kutoka Sh. 20,000 hadi 50,000 na uchumi ukikua mafanikio yanakwenda kwa walengwa na bila ya kukua kwa uchumi serikali haiwezi kutoa huduma kwa wananchi.
Alisema pia bajeti ya kusaidia wazee wasiojiweza imeongezeka, mambo hayo yanatekeleza mapinduzi yaliyokusudiwa kwa kusaidia wazee wasiojiweza na Rais wa Kwanza wa Zanzibar alijenga nyumba za kuwalea wazee.
Alisema uchumi wa Zanzibar unategemea zaidi sekta ya utalii ambao umeongezeka na kwa kipindi cha miaka minne uwekezaji katika sekta hiyo umeongezeka kutoka Dola za Kimarekani 784,947,180 na kufikia bilioni 382 na idadi ya watalii imeongezeka.
Alisema Dk. Mwinyi amesimamia elimu na idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 280,000 hadi 510,000 na kujenga shule 62 na madarasa zaidi ya 2000 kwa muda wa miaka minne.
Aidha, amejenga hospitali 10 za wilaya kila wilaya ina hospitali pamoja na hospitali mbili za mkoa.
Kuhusu uandikishaji wa wapigakura, alisema CCM inalengo ya kushinda uchaguzi na kukamata dola na kwamba ni wajibu wa wanachama kujiandikisha na kupiga kura katika uchaguzi mkuu na bila ya kupiga kura ushindi hautoweza kupatikana.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai akizungumza mchango wa jumuiya za chama hicho, alisema bila ya amani na utulivu nchini hakuna chochote kinachoweza kufanyika, viongozi wa nchi, Dk. Mwinyi na Dk. Samia pamoja na jumuiya za CCM wamesimamia kikamilifu kuwapo amani na utulivu.
Akizungumzia sekta ya elimu, Waziri wa elimu na mafunzo ya amali Lela Muhammed Mussa, alisema Dk. Mwinyi ameboresha mazingira rafiki ya kujisomea katika ngazi zote na kuwekeza fedha za kutosha kuhakikisha mazingira hayo yanafikiwa.
Alisema mwaka 2021 bajeti ya maendeleo katika sekta ya elimu ilikuwa Sh. bilioni 83.2, lakini kwa mwaka 2024 bajeti ni Sh. bilioni 518, kujenga madarasa 2,783, amejenga majengo ya shule ya ghorofa 35 ambazo zina maabara na maktaba za kisasa na zimeunganishwa na mkonga wa intaneti na wanafunzi kusoma kidijitali.
Akizungumza katika kongamano hilo, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema katika chaguzi zilizopita asilimia kubwa ya waliojiandikisha katika daftari la wapigakura huwa hawaendi kupiga kura na kutaka chama kuhakikisha watu wote wanaenda kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 wakati utakapofika.
Alisema uchaguzi ni kura hivyo ni vyema wananchi na wanachama kuhamasishwa kujiandikisha katika daftari la wapiga kura katika awamu ya pili katika daftari hilo na kila mwenye sifa kujiandikisha ili kuwa na sifa ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu.
Alisisitiza suala la amani na utulivu maana bila ya amani mafanikio yasingepatikana ambapo uchumi wa Zanzibar umekuwa kwa kiwango kikubwa.
Aidha, katika miaka minne ya uongozi wake amevuka malengo ya ilani ya CCM kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo sekta ya afya, elimu na miundombinu ya barabara.
Naye Makamu Pili wa Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu, Hemed Suleiman Abdullah, alisema Rais Dk. Mwinyi ameleta maendeleo makubwa kwa wananchi ikiwamo afya, elimu, miundombinu ya barabara na sekta nyengine.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mohammed Said Mohamed (Dimwa), alisema chama kinafarajika kuona Rais Mwinyi anafanya mambo mazuri kama aliyepewa dhamana ya uongozi katika kutekeleza ahadi kwa wananchi.
Alisema ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 ibara ya 135 waliahidi katika kipindi cha miaka mitano ya awamu ya serikali ya CCM itawaletea Wazanzibari misingi imara ya kiuchumi na kijamii, utawala bora na kuimarisha huduma za kijamii ambapo utekelezaji wa hayo unakwenda sambamba na malengo ya maendeleo ya mwaka 2050 na mikakati mbalimbali ya maendeleo ya miaka mitano.
Alisema CCM inaendelea kuamini kwamba Dk. Mwinyi ndio atakayekuwa mgombea wao kwa Zanzibar na Dk. Samia kwa Tanzania bara kwa 2025 na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za kimaendeleo wanazozifanya.
Mwenyekiti wa Wazazi Taifa, Fadhili Rajab Maganya, alisema mambo yote ya kimaendeleo yaliyofanywa na Rais Mwinyi ndio yameifanya jumuiya ya wazazi kumpongeza.
Alisema siku hiyo ni muhimu wanapoadhimisha miaka minne ya utumishi wake uliotukuka na amekuwa kinara katika kusimamia miradi ya kimaendeleo na jumuiya hiyo haina budi kumpongeza na kumwombea kila la heri.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED