Che Malone aitakatisha Simba Mbeya ikizoa tatu

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 08:42 AM Oct 23 2024
Beki wa Kati wa Simba, Che Malone Fondoh, akiifungia timu yake bao pekee baada ya kipa wa Tanzania Prisons, Musa Mbisa, kuutema mpira uliopigwa na Kibu Denis, kwenye mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya jana.
Picha:Mpigapicha Wetu
Beki wa Kati wa Simba, Che Malone Fondoh, akiifungia timu yake bao pekee baada ya kipa wa Tanzania Prisons, Musa Mbisa, kuutema mpira uliopigwa na Kibu Denis, kwenye mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya jana.

BAO pekee la dakika ya nne ya mchezo lililofungwa na Beki wa Kati, Che Malone Fondoh, jana lilitosha kuipa Simba pointi tatu mbele ya Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Ushindi huo umekuja siku tatu tu baada ya kutoka kupoteza mchezo wa dabi dhidi ya Yanga ambao Simba walikubali kipigo cha bao 1-0.

Katika mchezo wa jana, Che Malone aliifungia Simba bao hilo akitumia makosa ya golikipa wa Tanzania Prisons ambaye mpira uliopigwa na Kibu Denis ulimponyoka na kumpa nafasi mfungaji kuukwamisha nyavuni.

Simba jana walionekana kuutaka ushindi huo kutokana na kucheza kwa nidhamu kubwa kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa mchezo.

Ushindi huo wa jana unaifanya Simba sasa kufikisha pointi 16 baada ya kucheza michezo saba nakupanda mpaka nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.

Katika mchezo wa jana, Kocha wa Simba, Fadlu Davids, aliwaanzisha Fabrice Ngoma na Augustine Okajepha wakichukua nafasi ya Abdulrazaq Hamza na Yusuph Kagoma ambao hawakuwa sehemu ya kikosi cha kwanza baada ya kupata majeraha katika mchezo uliopita dhidi ya Yanga.

Simba jana walifanya mashambulizi kadhaa ambayo hata hivyo hayakuwapa nafasi ya kuongeza idadi ya mabao ambapo katika dakika ya 63 na 53 walikosa mabao kupitia kwa Edwin Balua aliyeingia katika dakika ya 61 kuchukua nafasi ya nahodha, Mohamed Hussein 'Tshabalala'.

Awali, Ateba alikaribia kuipa Simba bao la pili katika dakika ya 58 kabla ya kutolewa dakika ya 72 na nafasi yake kuchukuliwa na Steven Mukwala mabadiliko ambayo yaliongeza kasi ya mashambulizi, lakini hawakufanikiwa kupata bao lingine.

Tanzania Prisons ilijibu mapigo kwa nyakati tofauti kipindi cha pili, lakini umakini wa safu ya ulinzi ya Simba uliwanyima nafasi ya kupata bao la kusawazisha.

Dakika ya 76 Mukwala alikosa bao baada ya mpira wake wa kichwa akiunganisha faulo ya Mutale kutoka juu kidogo ya goli.

Simba walifanya mabadiliko mengine dakika ya 83 baada ya kumtoa Ladack Chasambi na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Muzamiru Yassin, hata hivyo mabadiliko hayo hayukubadilisha matokeo.

Katika mchezo huo, Kibu ambaye alikuwa tishio kwa mabeki wa Yanga mchezo uliopita, aliendelea moto wake jana kwa kuitesa ngome ya Prisons mara kwa mara kwa dakika zote 90 za mechi hiyo.

Ushindi huo licha ya kuihakikishia Simba pointi tatu, lakini pia wamelipa kisasi cha kufungwa kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu uliopita.

Kwa matokeo hayo pia yanaifanya Prisons kubaki katika nafasi ya 12 huku Simba ikipanda mpaka nafasi ya pili nyumba Singida Black Stars yenye pointi 19, lakini ikiwa na michezo miwili zaidi.

Singida Fountain Gate inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi sawa na Simba, lakini pia ikizidiwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa, Yanga ambayo jana jioni ilitarajiwa kucheza mchezo wao wa saba inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 15.