Tume ya Rais ya Maboresho Kodi yaanza kupokea maoni

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:18 AM Oct 23 2024
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, Balozi Ombeni Sefue, akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati akitoa taarifa kwa wananchi kuanza kazi kwa tume hiyo.
PICHA: SELEMANI MPOCHI
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, Balozi Ombeni Sefue, akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati akitoa taarifa kwa wananchi kuanza kazi kwa tume hiyo.

TUME ya Rais ya Maboresho ya Kodi imetangaza kuanza kukusanya maoni ya wadau, wakiwamo Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora).

Mifumo iliyoandaliwa kwa ajili ya kupokea maoni hayo ni pamoja na kiunganishi cha edodoso.gov.go.tz kwa kutumia namba ya dodoso 54497, barua pepe [email protected] na [email protected] au kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi za 0748 755 677 na 0738 588 813.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue alisema jana Ikulu, Dar es Salaam wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuwa: “Tunapenda kuwajulisha wananchi kuwa tume imeanza kazi na sasa iko tayari kushirikiana na kumsikiliza kila mdau, iwe mmoja mmoja au kupitia vyama vya kitaaluma, jumuiya za biashara na makundi mengine.

“Tume imeandaa namna bora ya kuratibu ushiriki wa wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za umma na binafsi, asasi za kiraia, wadau wa maendeleo, diaspora na wadau wote ili kutoa maoni na mapendekezo."

Balozi Sefue alisema watafanya mikutano na wananchi katika maeneo mbalimbali na kukutana na wawakilishi wa makundi. Alitoa  wito kwa taasisi za elimu ya juu, utafiti na nyingine zinazoweza kuandaa mijadala kuhusu hayo wawasiliane na tume.

Pia alitoa wito kwa vyombo vya habari kuandaa majukwaa ya majadiliano kuhusu maboresho ya mfumo wa kodi kisha kuandaa taarifa ambazo zitasaidia tume katika utekelezaji wa jukumu hilo.

Balozi Sefue alitoa wito kwa wananchi kutumia fursa hiyo adhimu kutoa maoni kuhusu changamoto na mapendekezo ya maboresho ya mifumo ya kodi na ukusanyaji wa mapato.

Alisema lengo ni mapendekezo yatakayowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan yaakisi uzoefu na maoni ya kila mwenye mchango wa kutoa katika kuboresha mfumo katika nchi.

Alisema tume hiyo imeundwa kutokana na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kuhusu kero zinazotokana na mfumo wa kodi nchini.

“Kodi ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani. Rais Samia ameonesha utashi wa kisiasa wa kushughulikia changamoto hizo na hatua ya kwanza ni kufanya tathmini ya kina ya mfumo ulioko ili kuwa na msingi wa kufanya maboresho ambayo ni wazi yanahitajika,” alisema.

Balozi Sefue alisema tume itasaidia kufanya tathmini hiyo kwa kushirikiana na wananchi wengi iwezekanavyo ili kuainisha changamoto zilizoko hasa umuhimu zaidi ni kukusanya mapendekezo yanayotekelezeka na yatakayosaidia kuongeza mapato ya serikali kwa njia iliyo rafiki na rahisi zaidi.

Balozi Sefue alisema katika kipindi cha miama mitatu iliyopita, pato halisi la taifa limekua kwa wastani wa asilimia 4.7, huku mapato ya kodi yakifikia wastani wa asilimia 12.1 ya pato la taifa.

“Kwa kawaida tungetarajia kasi ya ukuaji huu wa uchumi iendane sambamba na kasi ya ongezeko la mapato ya  serikali.

“Lakini hali si hivyo, kiwango tulichokifikia cha asilimia 12.1 ya pato la taifa ni chini ya asilimia 15 ya pato la taifa inayohitajika katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ili kujenga uwezo wa kufikia malengo ya kimataifa ya maendeleo endelevu,” alisema.

Alisema serikali imedhamiria kufikia kiwango hicho cha asilimia 15 ya pato la taifa ifikapo mwaka 2026/27 akitaka kuwa ni hatua itakayoongoza uwezo wa nchi kugharamia miradi ya maendeleo na kupunguza kiwango cha utegemezi wa mikopo na misaada.

Oktoba 4 mwaka huu, Rais Samia alizindua rasmi Tume ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Maboresho ya Kodi nchini. Tume itakusanya maoni kwa miezi miwili au mitatu.