Zanzibar Marathon kuchochea uchumi

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 08:57 AM Oct 23 2024
Mkurugenzi wa Tigo Zantel Kanda ya Zanzibar, Azizi Saidi Ali.
Picha;Mtandao
Mkurugenzi wa Tigo Zantel Kanda ya Zanzibar, Azizi Saidi Ali.

MSIMU wa pili wa mashindano ya Riadha ya Tigo Zanzibar Marathon unatarajiwa kufanyika Novemba 3, mwaka huu, Unguja, Zanzibar.

Mbio hizo zinatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa buluu kutokana na kuhusisha wanariadha mbalimbali wa nje na ndani ya Tanzania.

Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi wa Tigo Zantel Kanda ya Zanzibar, Azizi Saidi Ali, alisema mbio hizo zitakuwa za kilomita tano, 10 na 21 na zitasaidia kuibua vipaji, kukuza uchumi na kuimarisha afya za wananchi.

"Maandalizi yote muhimu yanaendelea na yapo hatua za mwisho, tumeongeza vituo vya kujiandikisha kwa watu wanaotaka kushiriki, lakini pia kwa mwaka huu tumerahisisha usajili ambapo mtu anaweza kujisajili kwa njia ya simu," alisema Ali.

Aidha, alisema pia wameboresha zaidi mbio hizo na kuwataka wanariadha na wapenda mchezo huo kujitokeza kwa wingi kushiriki.

Mmoja wa wadau wa mbio hizo, Hussein Juma Khamis, ambaye ni mwongoza watalii Zanzibar, alisema mbio hizo zinawaongezea nafasi za kuongeza kipato.

"Wakati wa mashindano haya wageni wanaongezeka sana hapa Zanzibar...tunapata fursa ya kipato katika sekta mbalimbali," alisema Khamis.

Aidha, Anwar Ali Salim ambaye ni dereva wa magari ya watalii, alisema wanasubiri kwa shauku kubwa mbio hizo maarufu Zanzibar.

"Mbio hizi pia zinasaidia washiriki kuimarisha afya, kukimbia ni dawa, watu tujitokeze kwa wingi kushiriki," alisema Ali Salim.

Mwaka jana mashindano hayo yalifanyika kwa mafanikio makubwa na kuhusisha mamia ya wanariadha.