RIPOTI MAALUMU -3 MIKOPO MTANDAONI Polisi yakiri vilio vingi, TCRA yadai 'haituhusu'

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:28 AM Oct 23 2024
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, DCP David Misime.
Picha: Mtandao
Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, DCP David Misime.

Sehemu ya pili ya ripoti hii jana ilikuwa na ushuhuda wa wananchi walivyorejesha mikopo kwa riba kubwa na hata kudhalilishwa na wakopeshaji wa mtandaoni. Endelea na sehemu ya mwisho…

 ---
UCHUNGUZI wa Nipashe umebaini baadhi ya namba za simu zinazotumika kudhalilisha wakopaji hazina utambulisho wa Tanzania, yaani ZIP CODE +255.

Katika ufuatiliaji wake, mwandishi alibaini kuwa kwa siku mtu mmoja anaweza kupigiwa simu na watu 10 tofauti wakizungumza jambo tofauti juu ya mkopo aliochukua.

 Baadhi ya namba zinazotumika kuwapigia simu wakopaji ni pamoja na zenye utambulisho (ZIP CODE) +212; +231; +355; +265; +216; +237; +248; +508; +467; +269;+257; +417; +324; +923; +236 na +882.

Ilibainika pia wakati wa uchunguzi kuwa mkopaji anaweza kupigiwa kwa namba ileile mara nyingi, lakini namba ya utambulisho (ZIP CODE) inabadilika. 

Mwandishi alirekodi jumla ya namba 25 baada ya watu wake wa karibu kukopa kuchukua mkopo mtandaoni.
 Mmoja wa vijana walioajiriwa na moja ya taasisi inayotoa mikopo hiyo (jina lake tunahifadhi) alisema: "Sisi tumeajiriwa tunalipwa ujira kwa kadri ulivyoingiza. Inabidi umsumbue mtu hadi aone kero alipe fedha anayodaiwa.

"Unakuta alishalipa lakini tunaambiwa lazima alipe na nyongeza, tunawaundia makundi maana wakati wa kuchukua mkopo wanaridhia tuone mawasiliano yao yote." 

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, DCP David Misime anathibitisha kuna malalamiko mengi yamefikishwa polisi kuhusiana na mikopo inayotolewa mtandaoni.

"Kuna malalamiko mengi sana. Mfano, kuna walioomba kukopa Sh. 500,000, wakapewa fedha pungufu, lakini wanapaswa kulipa mkopo wa Sh. 500,000 pamoja na riba.
 "Wengine wamefikia mahali anapoingia mkataba anaambiwa tuma kiasi fulani kwanza. Mfano, anakopa Sh. 400,000 anaambiwa tuma Sh. 50,000 kwa ajili ya kugharamia mkopo, lakini baada ya muda ile application inapotea.
 "Mtu anaposhindwa kurejesha mkopo, wakopeshaji wanasambaza ujumbe 'mkumbushe fulani anadaiwa vinginevyo hatua zitachukuliwa'," anasema.

Kamanda Misime anaonya kuwa huo ni unyanyasaji kwa kuwa wakati mtu anakopa hakumshirikisha anayetumiwa ujumbe; mkopeshaji anapotuma ujumbe wa aina hiyo ni kuvunja sheria.
 Julai mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alitoa bungeni maelekezo kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kitendo cha Uhalifu wa Mtandaoni, kufuatilia na kuchunguza watu wanaotumia taarifa za waliowakopesha mtandaoni kudhalilisha.

Vilevile, Juni 4 mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Emmanuel Mkilia, alionya taasisi na watu binafsi wanaofanya vitendo vya udhalilishaji kwa kuchukua taarifa za wateja wao, akisisitiza kuwa ni kinyume cha sheria.

Fedha za Kitanzania.

Mkuu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Tume hiyo, Innocent Mungy, anasema wananchi wengi hawana uelewa wa kulinda taarifa binafsi.

"Aliyesajiliwa anajua kuna kanuni, ila wengi hawazifuati na tumebaini wanatumia taarifa za watu kuwadhalilisha au kupeleka taarifa binafsi kwa ndugu na marafiki. Hili ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya Mwaka 2022," anaonya.

Mungy anasema kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo, wakopeshaji wanatenda makosa mawili: Mosi, kuendesha shughuli zao mtandaoni pasi na kusajiliwa na pili, kutumia taarifa binafsi za watu na kuziweka mtandaoni kwa nia ya kuwadhalilisha na kuondoa haki ya faradha.

Anabainisha kuwa hadi sasa waliosajiliwa ni 580 na ambao wako kwenye mchakato ni 688. Malalamiko 28 yaliyopokewa, yako kwenye hatua mbalimbali za kusikilizwa.

Mjumbe wa Bodi ya Tume hiyo, Maxence Melo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forums, anasema zimeibuka App nyingi zinazotoa mikopo, lakini asilimia 90 wamemchukulia mwananchi kama fursa ya kunufaika na si mteja wa kuhudumiwa.

"Jamii Forums tumepokea malalamiko zaidi ya 800 taarifa zao kuibwa, makato makubwa, watu wanapata mkopo kwa dakika chache, ukishapata unageuka mtu anayejutia, wanasambaza picha zako, wanavunja haki ya faragha na Sheria ya Taarifa Binafsi, hii ni mbaya sana," anasema Melo.

Anashauri mamlaka zisiishie kukemea tu, bali wakamatwe na wananchi wawekewa utaratibu wa kidigitali ili watoe taarifa na ushahidi wa taarifa zote zilizochukuliwa, isiwe lazima kwenda Dodoma au ofisi za Tume ya Taarifa binafsi.

Katika uchunguzi wake, mwandishi wa Nipashe alijisajili kwenye app ya CashX ambako alitakiwa kuwa na namba ya utambulisho wa uraia (NIDA), picha, majina matatu, tarehe ya kuzaliwa, majina ya wadhamini wawili ambao lazima ataje uhusiano wake na watu hao, namba zao za simu na namba ya nyumba wanakoishi.

Mwandishi pia alitakiwa kutaja kiwango chake cha elimu, kazi anayofanya, hali ya ndoa yake, kipato chake kwa mwezi, siku ya malipo na barua pepe.
 
 Pia walimtaka mwandishi atoe rukhsa rekodi ya simu yake kuhifadhiwa na wakopeshaji hao, wakiwa na maelezo: "Tutafuatilia tu ikiwa una rekodi za simu ili kuchanganua ikiwa unazitumia katika mazingira halisi ya kuzuia ulaghai. Tutahifadhi kwenye seva binafsi ya faragha na kuahidi kutoshiriki na mtu mwingine.
 
 "Kuhusu eneo, tunafuatilia anwani ya IP pekee. Tutaihifadhi kwenye seva ya faragha na kuahidi kutoishiriki na mtu mwingine."

Kwenye kamera waliandika: "Tunahitaji kuthibitisha maelezo ya utambulisho wa mtumiaji na maelezo yanayohusiana ili kutusaidia kujua zaidi kuhusu watumiaji (KYC). Tutahifadhi kwenye seva binafsi na kuahidi kutoishirikisha na mtu mwingine."
 
 Kuhusu kalenda ya mkopaji, waliandika: "Tunahitaji ufikiaji ili tuweze kukumbusha kufanya malipo kwa wakati katika kipindi cha kurejesha mkopo. Kipengele hiki kimeundwa ili kuboresha mchakato wa ulipaji na matumizi yako. Ikiwa hutawasha rukhsa hii, hutaweza kutumia sehemu mahususi inayohusiana na rukhsa hii."
 
 Mwandishi alibaini kuwa mwombaji mkopo hawezi kuendelea na maombi yake ikiwa hatatoa rukhsa ya taarifa zake na anapokataa, huletewa ujumbe wa "Tafadhari tupe ufikiaji wa rukhsa yako ya simu kabla ya kutumia huduma zetu."
 
Agosti 19 mwaka huu, mwandishi aliwasilisha maswala TCRA akitaka kujua uhalali wa matumizi ya namba za simu zenye utambulisho (ZIP CODE) usio wa Tanzania zinazotumika kutoa mikopo na mtandaoni na kama app hizo zinatambuliwa na mamlaka hiyo.

Majibu yaliyotolewa na mamlaka hiyo ni haya: "TCRA inathibitisha kupokea maswali juu ya masuala ya mikopo mtandaoni. Tunapenda kutoa ufafanuzi kuwa masuala yote yanayohusu fedha, ikiwa ni pamoja na mikopo ya mitandaoni yanasimamiwa na BoT na masuala ya uhalifu mtandaoni yanashughulikiwa na Jeshi la Polisi Tanzania."