Akaunti zenye dola zabainika hazijaguswa kwa mwaka mzima

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:25 AM Apr 17 2024
Uhaba wa dola nchini.
PICHA: ECONOMIC CONFIDENTIAL
Uhaba wa dola nchini.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amebaini kuwapo akaunti za benki ambazo hazijatumika kwa zaidi ya mwaka mmoja amezitaja ni za Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), hali inayohatarisha serikali kupata hasara ya mamilioni ya shilingi.

Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2022/23, CAG Kichere anasema amebaini TAA ilikuwa inamiliki akaunti tatu za benki ambazo hazikutumika kwa zaidi ya mwaka mmoja ambapo hadi Juni 30, 2023, zilikuwa na kiasi cha dola za Marekani 209 pamoja na Sh. milioni 170.14.

Vilevile, CAG anasema amebaini TBA pia ilikuwa na akaunti dumavu 33 za benki ambazo hazikuwa zinatumika tangu mwezi Oktoba 2020 na kati ya akaunti hizo, saba zilikuwa na kiasi cha Sh. milioni 12.48 hadi Juni 30, 2023.

“Kwa maoni yangu, upungufu huu unadhihirisha usimamizi mdogo wa akaunti za benki, hali ambayo kwa upande mwingine, inaweza kuiweka serikali katika hatari ya kupata hasara za kifedha, matumizi mabaya ya fedha za umma na kuruhusu mianya ya ubadhirifu.

“Ninapendekeza serikali kwa kushirikiana na TAA na TBA pamoja na Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, ifunge akaunti zote zisizotumika ili kupunguza hatari ya hasara za fedha, matumizi mabaya ya fedha za umma na hatari ya shughuli za udanganyifu.

"Pia ninapendekeza serikali kuhakikisha TAA inaimarisha usimamizi wa miundombinu ya viwanja vya ndege na kuzingatia kanuni na hatua za usalama ili kulinda usalama wa wafanyakazi, abiria na uendeshaji wa viwanja vya ndege," CAG anawasilisha hoja yake.

TAA 217 ZATELEKEZWA

CAG pia amebaini taa 217 za uwanja wa ndege (AGL) zenye thamani ya Dola za Marekani 334,986.05 katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma zinazotumia nishati ya jua zilitelekezwa kwenye stoo ya uwanja huo baada ya kubadilishwa na uwanja kuanza kutumia taa zinazotumia nishati ya umeme.

Anaonesha wasiwasi hali ya taa hizo zilizotelekezwa inaweza kuwa mbaya kutokana  mambo mbalimbali kama vile ukosefu wa matengenezo na uharibifu unaoweza kutokea kutokana na utunzaji usioridhisha.

SIMU ZAONGOZA NDEGE

Vilevile, CAG anasema amebaini kwenye Uwanja wa Ndege Bukoba, wafanyakazi wa udhibiti wa ndege ardhini walikuwa wanatumia simu za mkononi kupokea taarifa za safari na kuwasiliana na Mnara wa Udhibiti wa Ndege ulioko Mwanza, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.