Hatima ya Naibu Rais Kenya mikononi mwa wabunge wa Seneti

By Allan Isack , Nipashe
Published at 07:57 AM Oct 09 2024
Bunge la Kenya.
Picha: BBC Swahili
Bunge la Kenya.

BAADA ya Bunge la Kitaifa la Kenya kupiga kura kumwondoa madarakani Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua,anasubiri kufikishwa mbele ya Bunge la Seneti la nchi hiyo ndani ya siku mbili.

Kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo,Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya, Moses Wetangula, ana siku mbili za kutoa taarifa kwa Spika wa Seneti kuhusu matokeo ya mchakato wa jana. 

Hata hivyo,Spika wa Seneti Amason Kingi, ndani ya siku saba atakuwa na wajibu wa kuwafahamisha maseneta.

Pia Bunge la Seneti litakuwa na siku 10 za kuwasilisha kesi dhidi ya Gachagua, ambayo huenda itaanza kusikilizwa Oktoba 22.

Akitangaza uamuzi wa Bunge, Spika Wetangula,alisema “Ibara ya 145 (2) ya Katiba inaweka kizingiti cha angalau theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge ili kuunga mkono hoja maalum ya pendekezo la kuondolewa kwa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya ili hoja hiyo itekelezwe,” Spika Moses Wetang'ula alisema.

“Kwa mujibu wa matokeo ya uamuzi wa hoja niliyoitangaza hivi punde, jumla ya wajumbe 281 wakiwa ni zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge hilo, wamepiga kura kuunga mkono hoja hiyo,” alisema.

Aidha katika historia ya taifa hilo,
Gachagua ndiye Naibu Rais wa kwanza wa nchini hiyo,kushtakiwa chini ya Katiba ya 2010.

Awali Naibu Rais huyo,alifika mbele ya Bunge na kuwasilisha ushahidi wake dhidi ya mashtaka 11 ya kumuondoa madarakani.

Kiongozi huyo wa Serikali wa nchi hiyo,mwenye wadhifa wa juu anakabiliwa na mashtaka mbalimbali ikiwemo ufisadi, kumhujumu Rais William Ruto na kuendeleza mgawanyiko wa kikabila.

Oktoba  Mosi mwaka huu, hoja maalum ya kumwondoa Gachagua ofisini kwa njia ya kumshtakiwa iliwasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.

Mutuse aliwasilisha tuhuma 11 dhidi ya Gachagua akimtuhumu kwa ufujaji wa fedha na kutumia wadhifa wake kutoa zabuni za serikali kwa kampuni zake.

Licha ya tuhuma hizo kutolewa  Gachagua, alishikilia alishikilia msimamo wake kwamba hana hatia akidai kuwa amekuwa akitetea maslahi ya Wakenya.

Vilevile siku moja kabla ya kufika bungeni, alisema; ''Sina nia ya kujiuzulu kutoka wadhifa wangu na nitapambana hadi mwisho.''

Kesi ya Gachagua,inaweza kutekelezwa katika kikao cha pamoja(cha seneti nzima) au kikao cha kamati, lakini kutokana na uzito wake, huenda kikawa kikao cha seneti nzima.

 Spika wa Seneti,ataongoza kesi hiyo, maseneta watapata nafasi ya kumhoji Gachagua huku mawakili wake,wakitarajiwa kuwahoji mashahidi waliowasilishwa na bunge.

Katika kesi hiyo,mmoja wa mashahidi hao, ni Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja.

Kadhalika baada ya kesi ya mashtaka katika Seneti, kura ya thuluthi mbili zitatosha kumtimua Naibu Rais kutoka ofisi yake, kulingana na utaratibu wa kumuondoa madarakani ulioainishwa chini ya Kifungu cha 150 cha Katiba.

Mbali na kumwondoa madarakani, Naibu wa Rais atasalia kwenye wadhifa wake, iwapo hoja hiyo itakataliwa na theluthi moja ya maseneta au iwapo Seneti itaunda kamati ambayo itapata sababu za kushtakiwa kukosa ithibati au msingi.

Naibu Rais pia atakuwa na haki ya kufika au kuwakilishwa mbele ya kamati maalum wakati wa uchunguzi dhidi yake.

Kamati Maalum inaweza kusikiliza hoja za mwakilishi au mbunge aliyewasilisha hoja hiyo katika Bunge na wajumbe wengine.

Ikiwa kamati maalum itaripoti kwamba maelezo ya tuhuma yoyote dhidi ya Naibu Rais hayajathibitishwa, mashauri mengine hayatachukuliwa chini ya Ibara ya 145 ya Katiba kuhusiana na madai hayo.

Iwapo yatathibitishwa, bunge la Seneti, baada ya Naibu Rais kupata nafasi ya kusikilizwa, litapiga kura kuhusu mashtaka dhidi yake.

Seneti itapiga kura ya 'ndiyo' na 'hapana' kwa kila shtaka dhidi yake.

Iwapo  theluthi mbili ya wanachama wote wa Seneti watapiga kura kuunga mkono shtaka lolote la kumshtaki, atalazimika kuchia nafasi yake

Ikiwa hayatathibitishwa, Naibu wa Rais ataendelea kushikilia wadhifa huo.