Aliyekuwa Rais wa Iran Raisi kuzikwa leo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:25 AM May 22 2024
news
Picha: Mtandaoni
Kaimu Rais, Mohammad Mokhber (katikati) akizungumza na vyomba vya habari awapo pichani.

ALIYEKUWA Rais wa Iran Ebrahim Raisi na wengine nane waliopata ajali ya helikopta juzi wanatarajia kuzikwa leo katika mji wa Tabriz alikokuwa akisafiri, na kwamba miili yao itapelekwa kwanza kwenye idara ya uchunguzi wa kitaalamu kabla ya maziko.

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisema jana kuwa kutakuwa na maombolezo ya kitaifa ya siku tano kwa lengo la kutoa heshima ya mwisho kwa hayati Rais Raisi.

Wakati huo huo Baraza la mawaziri nchini humo lilimteua Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Ali Bagheri Kani kuwa kaimu waziri wa mambo ya nje, baada ya kifo cha Hossein Abdollahian aliyekuwa waziri katika wizara hiyo.

Aidha, baada ya ajali hiyo maelezo zaidi yameanza kujitokeza yakieleza kilichotokea kwa mmoja wa abiria waliokuwemo ndani ya helikopta hiyo Mohammad Ali Al-Hashem, aliyekuwa Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Tabriz, mji ambao msafara huo ulikuwa unaelekea.

Kwa mujibu wa Mohammad Nami, Mkuu wa Shirika la Kudhibiti Migogoro ya Iran, Al-Hashem alinusurika kwa saa nzima baada ya ajali hiyo ambayo iliuwa watu wote tisa waliokuwa ndani ya helikopta. Na kwamba imam alijaribu hata kuwasiliana na ofisi ya rais bila mafanikio.

“Hakuna uchunguzi wa chembechembe za vinasaba, DNA iliyohitajika kubaini abiria,” Nami aliiambia BBC.

Ilielezwa kuwa Iran imeanza siku tano za maombolezo huku wananchi wakiandamana barabarani katika miji tofauti kote nchini humo, na kwamba mwili wa Rais Raisi utapelekwa kaskazini mashariki kuagwa, kasha kizikwa Mashhad kwenye kaburi la Imam Reza, mrithi wa nane wa Mtume Muhammad.

HAKIHARIBIKI KITU

Baada ya Kiongozi wa juu wa kisiasa na kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei kumtangaza kuwa kaimu Rais, Mohammad Mokhber aliongoza kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri. Akiwahakikishia raia wa taifa hilo kuwa hakuna kitakachoharibika baada ya kifo cha Ebrahim Raisi.

Akizungumza katika televisheni ya taifa hilo Kaimu Rais Mokhber, alisema kwamba watafuata njia ya Rais Raisi katika kutekeleza majukumu waliyopewa bila usumbufu wowote.

“Hili ni tukio zito la kusikitisha kwetu sote. Linasababisha huzuni na uchungu lakini kuhusu suala la utawala na mwenendo wa nchi, watu wote wanapaswa kuwa na uhakika kuwa hakutakuwa na tatizo lolote,” alisema Mokhber.

Hata hivyo, alisema nchi hiyo itaendelea kusonga mbele chini ya uongozi wake na kwamba kila mmoja anapaswa kuendelea na majukumu yake licha ya msiba huo. Akieleza kuwa kwa namna yoyote ile, kilichotokea hakipaswi kuingiliana na serikali na uendeshaji wa taifa la Iran.

Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo Mokhber, atahudumu katika nafasi ya kaimu rais wa Iran kwa kipindi cha siku 50 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi maalumu Juni 28, mwaka huu.

Ilieleza kuwa mchakato wa uchaguzi wa mrithi wa Rais Raisi utaanza na fomu zitawasilishwa kati ya Mei 30 na Juni 3, mwaka huu, na kwamba orodha ya wagombea walioidhinishwa inatarajiwa kuchapishwa Juni 11 na uchaguzi utafanyika Juni 28.

Hapo litajulikana jina la mrithi wa hayati Rais Raisi, pia ni ishara ya shauku ya walio madarakani kuonesha kuwa licha ya kifo cha kiongozi huyo, hakuna mgogoro wa kisiasa au kitaasisi unaoripotiwa.

KUHUSU HELIKOPTA

Wakati maelezo yakiendelea kujitokeza, vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilisema kwamba helikopta iliyombeba rais na waziri wa mambo ya nje ilikuwa aina ya Bell 212.

Vilevile, ilielezwa kuwa haijulikani helikopta hiyo ilikuwa imefanya kazi kwa muda gani, lakini aina hiyo ya helikopta ilitengenezwa kwa jeshi la Canada miaka ya 1960. Huku ikielezwa kwamba miongo kadhaa ya vikwazo vya Marekani na kimataifa vilianza baada ya mapinduzi ya Iran mwaka 1979.

Ilibainishwa kuwa helikopta hizo zilitengenezwa na kampuni ya ‘Bell Helicopter’ ya Marekani na kutumika sana na waendeshaji wa serikali, ikiwa ni pamoja na vyombo vya sheria vya Marekani na polisi wa kitaifa wa Thailand.

Ilielezwa kuwa Jeshi la Wanamaji na la anga la Iran lina jumla ya helikopta hizo 10, kwa mujibu wa nyaraka ya 2024 ya Jeshi la Anga la Dunia la ‘FlightGlobal’, lakini haijulikani ni ngapi zinatumiwa na serikali ya Iran hadi sasa. Na kwamba zinaweza kutumiwa kufanya mambo tofauti kama kubeba watu na mizigo, na zinaweza kuwekwa silaha kwa ajili ya kupigana.

Shirika la habari la serikali la IRNA linasema kuwa helikopta iliyombeba rais inaweza kubeba abiria sita na wafanyakazi wawili.

Kwa mujibu wa Wakfu wa Usalama wa Ndege, shirika lisilo la kiserekali, ajali ya hivi karibuni iliyohusisha ndege aina ya Bell 212 ilitokea Septemba 2023 wakati mwanamitindo aliyekuwa akiendeshwa kwa faragha ilianguka kwenye ufuo wa Falme za Kiarabu. Na nyingine ilitokea Aprili 2018, wakati Bell 212 ikiwa inamsafirisha mgonjwa aliyekumbwa na mshtuko wa moyo.

Chanzo mashirika ya kimataifa.