Watoto njiti, Wazazi SekouToure wapatiwa msaada kukidhi mahitaji

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:05 PM Oct 26 2024
Meneja wa benki ya Baroda (T) Tawi la Mwanza, Victoria Kavishe (kulia akikabidhi daipazi kwa mmoja wa akina mama waliojifungua watoto njiti katika Hospitari ya rufani Mkoa (Sekou Toure).
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja wa benki ya Baroda (T) Tawi la Mwanza, Victoria Kavishe (kulia akikabidhi daipazi kwa mmoja wa akina mama waliojifungua watoto njiti katika Hospitari ya rufani Mkoa (Sekou Toure).

WATOTO zaidi ya 50 waliozaliwa kabla ya muda ‘njiti’ pamoja na wazazi wao wenye uhitaji wanaopatiwa huduma katika Hospitali ya Rufani Mkoa wa Mwanza (Sekou Toure) wamepatiwa msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo mafuta ya joto, maziwa, sabuni, daipazi pamoja na vifaa vingine vya usafi hospitalini ili kukidhi mahitaji wakati wakipatiwa huduma.

Vifaa hivyo vimetolewa leo Oktoba 26,2024 na wadau wa maendeleo kutoa Banki ya Baroda (T) ltd, Tawi la Mwanza ikiwa ni sehemu ya kuadhimia miaka 20 ya kuanza shughuli zake nchini.

Akizungumza wakati wa kutoa vifaa hivyo, Meneja wa benki hiyo Tawi la Mwanza, Victoria Kavishe amesema hatua hiyo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na kuwakumbuka watu wenye uhitaji zaidi huku akiwataka wadau wengine kufanya hivyo au zaidi kwa watu wenye uhitaji wakiwemo yatima.

“Tumefikiisha miaka 20 toka tufungue benki yetu hapa Tanzania, hivyo tumeona ni jambo jema tusisherehekee wenyewe bali kwa kuwagusa wenye uhitaji kwa kutoa kitu kidogo kwa mama wenye watoto waliozaliwa kabla ya muda wao,”amesema Kavishe.

Aidha amesema msaada huo ni kwaajili ya watoto, wazazi pamoja na sambuni za kufanyia usafi kwaajili ya Hospitali ili kuhakikisha wanapata huduma katika mazingira rafiki.

Muuguzi wodi ya watoto wachanga katika hospital hiyo, Beatrice Kanja, amesema kwa siku hospitali hiyo inapokea watoto kuanzia 20 mpaka 50 huku baadhi yao wakiwa hawana uwezo wa kumudu mahitaji muhimu kama hayo hivyo kuwakumbusha watu mbalimbali kuwakumbuka pia.

“Sisi binafsi tunafarijika kuona wazazi na watoto wanapata mahitaji hivyo tunawashukuru kwa misaada hii itakayowasaidia kinamama hawa kuendelea kusukuma siku na kupinguza utegemezi kwa ndugu zao,”amesema Kanja.

Mmoja wa mama mwenye mtoto hospitalini hapo Alphonsina Angelo amesema hajuhi atatoka lini kulingana na hali yake licha ya kuwa na huduma zilizoboreshwa hospitalini hapo lakini mahitaji binafsi ndiyo yanakuwa gharama wakati wa  kupatiwa huduma.

Mzazi mwingine Christina Julius, alisema kununua vifaa vya namna hiyo ni ghali na mara nyingi wanashindwa kuwa navyo hivyo kupitia msaada huo wataweza kusukuma siku mpaka waka wa kuruhusiwa ukifika.