Mutembei: Mwanafunzi kidato cha nne atakayepata DIV 1.7 kushomeshwa bure

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 08:18 PM Oct 25 2024
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Victory.
Picha: Yasmine Protace
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Victory.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MUTEMBEI Holding Limited (MHL), Wakili Peter Mutembei, ametoa motisha kwa wahitimu wa kidato cha nne kwa kutangaza kwamba mwanafunzi atakayefaulu kwa daraja la kwanza kwa kupata pointi 7 atasoma bure kidato cha tano na sita katika shule yao ya St. Mathew’s.

Mutembei alitoa kauli hiyo wakati wa mahafali ya 17 ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Victory, iliyopo Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.

“Tuna shule tano za sekondari na shule tatu za elimu ya msingi na awali. Shule ya St. Mathew's ina elimu ya awali hadi kidato cha sita. Wanafunzi wa kidato cha nne wanaofaulu daraja la kwanza kwa kupata pointi 7 wataweza kusoma bure kidato cha tano na sita,” alisema Mutembei.

Aidha, alisisitiza kwamba shule zao zinasimamia malengo matatu makuu: malezi, elimu, na usalama. Aliongeza kuwa, shule hizo zinatoa udhamini kwa wanafunzi wenye vipaji na punguzo la ada kwa wazazi wenye watoto wengi katika shule zao.

Mutembei alisema kuwa walimu ambao wanafunzi wao watafaulu vizuri mitihani ya kitaifa atawapatia motisha ya fedha. Pia, aliongeza kuwa wameandaa ofa maalum kwa walimu, ambapo mwalimu atakayefundisha kwa miaka mitano mfululizo atapewa kiwanja ili kujenga nyumba.

1
Pia, Mutembei alimwomba Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga, Hassan Mwela, kuwapatia ekari 50 za ardhi ili kujenga Kijiji cha wafanyakazi wapatao zaidi ya 400.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ponsiano Mlelwa, alisema kuwa elimu wanayotoa kwa wanafunzi wao imezaa matunda, kwani kila mwaka ufaulu unakuwa mzuri na hakuna mwanafunzi wa kidato cha nne anayeshindwa.

Mlelwa aliongeza kuwa shule hiyo ina mpango wa kuachana na ufundishaji wa chaki na badala yake wanatarajia kufundisha kwa kutumia luninga.

“Kwa sasa tuna luninga moja, lakini tunahitaji luninga tano zaidi,” alisisitiza Mlelwa.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwafundisha wanafunzi kwa kuzingatia mahitaji yao, akisema kuwa wanawaandaa wanafunzi ili waweze kufanikiwa kimaisha. “Kila mtoto ambaye amekuwa akikataliwa katika shule nyingine, tunawachukua na kuwapa elimu bora, na hii imechangia ufaulu wa watoto hao,” aliongeza.

Mwisho, Mutembei aliwataka wahitimu kuwa makini na kumtumikia Mungu ili waweze kufanikiwa katika maisha yao.