Balozi akoshwa Tanzania inavyoimarisha uhusiano wa kidiplomasia

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:43 PM Oct 25 2024
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dk. Jim Yonazi akizungumza jambo wakati alipoambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Ummy, alipotembelea ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Namibia.
Picha: Ofisi ya Waziri Mkuu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dk. Jim Yonazi akizungumza jambo wakati alipoambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Ummy, alipotembelea ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Namibia.

KAIMU Balozi wa Tanzania nchini Namibia Elias Tamba anafurahishwa na namna Tanzania inavyoendelea kuimarisha misingi ya uhusiano wa diplomasia baina yake na nchi hiyo katika nyanja mbalimbali, huku mchango wa kusaidia uhuru wa Namibia ukitajwa.

Ameyamesema hayo wakati Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga, alipotembelea Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Namibia leo.

Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Namibia katika masuala mbalimbali kwa kuzingatia urafiki uliopo baina ya mataifa hayo mawili toka kipindi cha uhuru wa taifa hilo ambako Tanzania inakumbukwa kwa mchango wake.

"Naishukuru serikali ya Tanzania kwa namna inavyoendelea kuhakikisha inaimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina yake na Namibia, hii itasaidia kuchangamkia fursa za kimaendeleo zilizoko katika taifa hili ikiwemo masuala ya kibiashara," amesema.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga akizungumza alipotembelea ofisi za Ubalozi wa Tanzania Nchini Namibia. Picha Ofisi Waziri Mkuu.

Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Ummy, amesema hatua hiyo imefikiwa kutokana na uongozi makini wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyojipambanua kidiplomasia na kuhakikisha mahusiano ya Taifa na nchi nyingine unakuwa wenye manufaa na kuiletea nchi heshima katika nyanja mbalimbali.


“Hakika Tanzania imeendelea kuwa kitovu cha amani na utulivu, hii imetokana na uongozi mahiri wa Rais Samia kwa miongozo na maelekezo yake katika kuhakikisha nchi inaendelea kujipatia maendeleo,” amesema Ummy.